Breaking

Wednesday, 25 January 2023

MWALIMU ALIYEONEKANA AKIWAKANYAGA MIGUU NA KUCHAPA VIBOKO WANAFUNZI ASIMAMISHWA KAZI



Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Albert Chalamila ametoa ufafanuzi kuwa Mwalimu aliyeonekana katika video akipiga mwanafunzi viboko,yupo Wilaya ya Kyerwa, Mkoa wa Kagera,Kata ya Kakanja,shule ya Msingi Kakanja.

Tukio ni la kweli limetokea,tarehe 10.01.2023, ambapo Mwalimu huyo alipiga viboko wanafunzi zaidi ya mmoja, upigaji wake ndio ulioleta taharuki kwa umma ya Watanzania. Zaidi katika video ile kuna baadhi ya walimu waliokuwa pembeni walisikika wakicheka wakati mwalimu huyo akiwapiga wanafunzi.

Mwalimu aliyepiga viboko wanafunzi ni Mwalimu Isaya Benjamin Emmanuel, mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Kakanja na walimu walioonekana na kusikika kufurahia tukio hilo wakati mwalimu Mkuu akiwachapa wanafunzi hao walikuwa ni walimu wanne ambao ni Mwalimu Godson Rwabisho,Beatrice Oswald Kaburanyange,James Josiah na Delphina Leonce.

Wanafunzi waliochapwa ni Salmon Kakwezi darasa la nne umri wa miaka tisa na Anord Kweyamba darasa la nne umri miaka kumi. Mwalimu aliwachapa viboko wanafunzi kwasababu hawakufanya kazi ya nyumbani waliyopewa wakati wa likizo akaona adhabu kubwa ya kuwaadhibu ni kuwachapa wanafunzi namna alivyowachapa.

Kwa mujibu wa Waraka wa Elimu namba 24. wa Mwaka 2002 kuhusu adhabu ya viboko, ni kuwa itazingatia ukubwa wa kosa, umri, jinsi, afya ya mtoto na isizidi viboko vinne kwa wakati mmoja.

Kosa la kwanza la Mwalimu Isaya alipiga viboko zaidi ya vinne kinyume na Waraka wa Elimu, adhabu ya viboko itatolewa na Mwalimu Mkuu au Mwalimu mwingine atakayeteuliwa na Mwalimu Mkuu kwa maandishi kila mara kosa linalostahili adhabu hii litakapotendeka.

Mwalimu Mkuu alistahili kwakuwa ni mamlaka ya nidhamu ya kuadhibu lakini kosa lake ni aina ya upigaji wake ulikuwa ni wa kuwakanyaga wanafunzi miguu,kuwapiga kwenye miguu jambo ambalo lingeweza kupelekea kwa afya za wanafunzi hao.

Mamlaka yake ya Nidhamu,chini ya Katibu Tawala Mkoa tayari hatua za kinidhamu zimechukuliwa ambazo ni kutenguliwa Ualimu Mkuu, amesimamishwa kazi na Kamati za uchunguzi zinaendelea kuchunguza suala hili ili kupata uhalisia vigezo vinavyostahili ili aweze kuchukuliwa hatua stahiki ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Kwa niaba ya Uongozi wa Mkoa Mhe. Albert Chalamila ameomba radhi Watanzani kwa tukio hilo, ambalo linaumiza, kusisimua kadri unavyoona mtoto yule alivyopigwa na alianza kuchechemea.

Sambamba na hayo amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuchukua hatua za kisheria kwa Mratibu Elimu Kata na kuchunguza zaidi kuhusu ufanisi wake na ubora wake katika utendaji kazi.

Pia kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu ya miongozo ya Elimu, walimu ambao walitarajiwa kuwa walezi, washauri wa Mkuu wa Shule lakini kinyume chake wakaonekana na wao kutofanya jukumu lao na kucheka na kukiuka jukumu la kuwa Walezi na Washauri wa Mwalimu Mkuu

Ameeleza kuwa inawezekana moja ya kigezo kinachopelekea wanafunzi wasiripoti haraka shuleni ni pamoja na adhabu za aina hiyo ambazo zinakiuka misingi ya haki za binadamu.

"Tukio hilo lililotokea tarehe 10.01.2023 lilitarajiwa walezi na wasimamizi wa shule au Kamati ya shule na Kata waweze kuchukua hatua hizi haraka Na endepo walichelewa kupata taarifa inadhihirisha namna gani hawatembelei shule zao, hawazungumzi na walimu na hawazungumzi na wanafunzi."

Amesisitiza wazazi, walezi na viongozi ngazi za kata kutembelea shule, kufanya vikao vya mara kwa mara na wazazi na walimu zaidi wabebe jukumu la kulea kwa mujibu wa kanuni na taratibu ya kazi zao ila wasikiuke na kupoteza mwelekeo wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwaendeleza watoto akiamini ndio nguvu kazi ya kesho.




Via Kagera Rs
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages