Breaking

Wednesday, 4 January 2023

MMILIKI WA MOCHWARI AHUKUMIWA MIAKA 20 JELA KWA KUUZA VIUNGO VYA MAITI 560



Mmiliki wa zamani wa mochwari katika Jimbo la Colorado, Marekani, amehukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani kwa kuwalaghai jamaa za waliofariki na kuuza viungo vya miili ya maiti 560 bila idhini.

Megan Hess, 46, aliungama makosa ya ulaghai mnamo Julai 2022, akiendesha hifadhi ya maiti ya Sunset Mesa.


Hess pia alikuwa anamiliki shirika la kutoa huduma za mchango wa viungo vya mwili kutoka jengo moja mjini Montrose, Colorado.

Alihukumiwa kifungo cha miaka 20 mnamo Jumanne, Januari 3, ambacho ndicho kinruhusiwa chini ya sheria ya taifa hilo.

Mamake Hess, mwenye umri wa miaka 69, Shirley Koch, pia alikiri kosa la ulaghai na alihukumiwa kifungo cha miaka 15.

Mahakaa iliambiwa kuwa jukumu kuu la Koch lilikuwa kukatakata miili.

"Hess na Koch walitumia mochwari yao wakati mwingine kuiba miili na viungo vya mwili kwa kutumia fomu za wafadhili za ulaghai na ghushi," mwendesha mashtaka Tim Neff aliambia mahakama akiongeza kuwa tabia ya Hess na Koch ilisababisha uchungu mkubwa kwa familia za waathiriwa.

Jaji wa Wilaya ya Marekani Christine M. Arguello akitoa uamuzi wake alisema kuwa kesi hiyo ilikuwa ya kuhuzunisha zaidi hajawahi kukumbana nayo kortini. Arguello aliamuru kwamba Hess na Koch wapelekwe gerezani mara moja.

Kesi hiyo ilichochewa na ripoti ya udukuzi wa Shirika la Habari la Reuters katika kipindi cha mwaka 2016-2018 kuhusu uuzaji wa sehemu za mwili nchini Marekani.

Wafanyikazi wa zamani waliambia Reuters kwamba Hess na Koch waliendesha biashara haramu ya kupasua miili bila idhini na wiki chache baada ya taarifa hiyo kupeperushwa mnamo mwaka wa 2018, FBI ilivamia makafani hayo.

Katika Mochwari yake, Hess alikuwa akitoza familia hadi $ 1,000(KSh123,000) akiwalaghai kuwa ni ya uchomaji wa maiti ambao haujawahi kutokea.

Waendesha mashtaka walisema alidanganya zaidi ya familia 200, ambazo zilipokea majivu yaliyochomwa kutoka kwa mapipa yaliyochanganywa na mabaki ya maiti tofauti.

Ni kinyume cha sheria nchini Marekani kuuza viungo vya mwili kama vile mioyo na figo kwa ajili ya kupandikiza.

Lakini kuuza sehemu za mwili kama vile vichwa, mikono na uti wa mgongo kama alivyofanya Hess, kwa matumizi ya utafiti au elimu, hakudhibitiwi na sheria.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages