Breaking

Tuesday, 3 January 2023

MAMA ATUHUMIWA KUUWA WATOTO WAKE WAWILI NA KUWEKA MIILI YAO KWENYE NDOO



Mama wa watoto wawili waliouawa katika Kijiji cha Kerwa eneo la Kikuyu nchini Kenya usiku wa mkesha wa mwaka mpya, amekamatwa.

Wawili hao, mvulana wa miaka saba na msichana wa miaka mitano walipatikana wamekufa katika nyumba ya familia yao huko Kikuyu.

 Kulikuwa na tuhuma kwamba mvulana huyo aliteswa kabla ya kifo chake kisichotarajiwa kulingana na Kamanda wa Polisi wa Kikuyu Catherine Ringera.

"Maafisa wa polisi walimpata mvulana huyo akiwa amefungwa mikono na kichwa chake kikisukumwa kwenye ndoo iliyojaa maji."

 "Ingawa mikono ya msichana huyo haikuwa imefungwa, vile vile aliingiza kichwa chake kwenye ndoo ya maji," alisimulia.

 Hata hivyo, badala ya mama huyo kuripoti tukio hilo kwa askari polisi, alikwenda kumweleza mumewe ambaye anafanya kazi umbali wa kilomita mbili.

 "Tumemkamata mama ili kutusaidia katika uchunguzi," Ringera alifichua.

 Miili ya watoto hao wawili ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Thogoto ikisubiri uchunguzi wa maiti.

Ringera alisema kuwa watatafuta maagizo ya korti kumzuia mama huyo zaidi ili kukamilisha uchunguzi wa mauaji hayo ya kutisha.

OCPD alisema walipata simu ya mwanamke huyo ambayo ilikuwa na skrini iliyovunjika na ujumbe ambao alimtaka mume wake amlipe madeni yake.

Ringera aliongeza kuwa wamekusanya sampuli kutoka eneo la tukio ikiwa ni pamoja na vitabu vitakavyosaidia kuwakamata waliohusika katika mauaji hayo.

Kulingana na jirani aliyezungumza na vyombo vya habari, mama huyo alikana kuhusika kwa vyovyote vile.

 "Mama huyo alituambia kwamba alisikia mlango ukigongwa na alipofungua, mtu alimpiga na kitu butu," jirani huyo aliambia wanahabari.

 Kulingana na jirani huyo, mama alipopata fahamu, alipata watoto wake wawili wameuawa bafuni.

Mwanamke huyo atafikishwa kortini leo, Jumanne, Januari 3 akisubiri uchunguzi zaidi wa polisi.

Baba ya watoto hao Paul Gaitho, ambaye ni mchinjaji alisema alipata simu ya kutatanisha kwamba watoto wake wawili walikuwa wametekwa nyara na watu wasiojulikana.

Alisema kwamba aliacha kazi yake akifuatana na marafiki zake na kukuta watoto wake tayari walikuwa wameuawa na kutupwa bafuni; mmoja akiwa amefungwa kamba ya kiatu, na mwingine ametupwa kwenye ndoo ya maji.

"Niliambiwa watoto wamekuwa hijacked. Nilitoka na marafiki zangu tukaenda hadi kwa nyumba. Nilikuta kama watoto washauwawa," alisema Gaitho.

Mama huyo anaripotiwa kuwa pekee yake na watoto ndani ya nyumba wakati shambulio hilo linalodaiwa kutokea.

Alikimbia umbali wa kilomita mbili ambapo alimfahamisha jirani yake kwamba alishambuliwa na hakujua waliko watoto wake.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages