Ofisi ya Rais - TAMISEMI inatarajia kuanzisha ushirikiano na Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JKMF) unaolenga kuanzisha mpango maalum wa kutoa ajira ya muda mfupi kwa walimu wa kujitolea watakaofundisha Shule za msingi za Serikali kwa kipindi kisichopungua miaka miwili.
Ushirikiano huo umejadiliwa leo katika kikao cha pamoja kati ya Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya JMKF na Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI kilichofanyika Dodoma leo tarehe 27 Januari 2023.
Katika kikao hicho, pamoja na mambo mengine , Mhe. Dkt. Kikwete ameishauri Ofisi ya Rais TAMISEMI kutengeneza kanzidata ya Walimu wote wanaojitolea nchini na kuandaa muongozo utakaosimamia mchakato wa kuwapata walimu wa kujitolea na kuratibu maslahi yao.
Mhe. Dkt. Kikwete ameelezea utayari wa Taasisi ya JMKF kushirikiana kwa karibu na Serikali kutekeleza mpango huo ambao tayari Taasisi hiyo imejipanga kuanza kuutekeleza kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) na wadau wengine.
Kupitia kikao hicho, Mhe Dkt Kikwete aliomba Serikali iweke utaratibu mzuri wa kuwaajiri walimu wa kujitolea watakaomaliza muda wao wa kujitolea ili kufanya mpango huo uwe endelevu.
Waziri Mhe. Angellah Kairuki alimweleza pia Mhe. Dkt. Kikwete kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI imejipanga kuboresha sekta ya elimu kwa kuanzisha utoaji elimu kidijitali kwa kuanzisha maabara za TEHAMA *na sayansi* katika shule zote za Serikali hapa nchini, ambapo kwa kuanzia shule mpya zote zinazojengwa *zitakuwa na maabara ya sayansi* na zitaunganishwa na mfumo wa intaneti ili kufikia lengo hilo.
Aidha, Waziri Angellah Kairuki amepongeza Taasisi ya JMKF kwa kuanzisha programu ya kutoa elimu kidijitali na kwa kuwa tayari kushirikiana na Serikali katika eneo hilo.
Waziri Kairuki alihitimisha kwa kuishukuru Taasisi ya JMKF kwa jitihada zake za kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita katika kuendeleza na kuboresha sekta ya elimu nchini na ameahidi kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Taasisi hiyo na wadau wengine wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo wanaoiunga mkono Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu.