Shirika la Fedha Ulimwenguni IMF limesema kuwa uchumi wa dunia utakabiliwa na wakati mgumu zaidi mnamo mwaka huu wa 2023, wakati ambapo mataifa makubwa yakishuhudia shughuli zao zikidhohofika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Kristalina Georgieva ameeleza kuwa theluthi moja ya uchumi wa dunia itadorora zaidi mwaka huu
"Tunatarajia theluthi moja ya uchumi wa dunia kudorora," Georgieva aliuambia mtandao wa TV wa Marekani CBS katika mahojiano yaliyopeperushwa Jumapili, akiongeza kuwa "nusu ya Umoja wa Ulaya itakuwa katika mdororo mkubwa"
Amesema sababu kubwa ni mataifa matatu yenye uchumi mkubwa Marekani, China na yale ya Umoja wa Ulaya kwa pamoja yanakabiliwa na kasi ndogo ya ukuaji uchumi.
Hapo Oktoba, IMF ilisimamisha ubashiri wake wa ukuaji wa uchumi wa dunia kwa mwaka 2023.
Uchumi ulionyesha kuendelea kudorora kutokana na vita vya Ukraine pamoja na shinikizo la mfumuko wa bei na viwango vya juu vya riba vilivyowekwa na benki kuu kama vile Benki Kuu ya Marekani inayolenga kuondoa msukumo wa mfumuko wa bei.