Breaking

Tuesday, 24 January 2023

DKT. KIKWETE KUENDELEA KUCHANGIA HUDUMA ZA UZAZI, MAMA NA MTOTO


Na. WAF, Dar es Salaam

Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto ni suala ambalo lipo ndani ya moyo wake na ataendelea kutoa mchango kwa Serikali na wananchi kwa ujumla.


Dkt. Kikwete ameyasema hayo wakati alipotembelewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi ofisini kwake jijini Dar es Salaam.


Dkt. Kikwete amesema anaishukuru Serikali kupitia Wizara ya afya kwa kuendelea kumwamini na kumtumia katika mchango wake wa kuboresha huduma katika sekta ya afya nchini.


Naye, Katibu Mkuu,Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi ametoa shukrani za dhati kwa Rais Mstaafu Dkt. Kikwete kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya Afya alipokuwa Rais na baada ya kustaafu hususan katika eneo la afya ya msingi, rasilimali watu, mafunzo ya kibingwa, afya ya mama na mtoto, huduma za meno na uwekezaji mkubwa katika Hospitali ya JKCI, Mlonganzila, Benjamin Mkapa na Chuo kikuu cha CUHAS.


Aidha, hadi sasa Rais Mstaafu anaendelea kutoa ushirikiano yeye binafsi na taasisi yake ya Jakaya Mrisho Kikwete Foundation kwa Wizara ya afya katika jitihada za kuboresha huduma za afya hususani huduma za Uzazi, Mama na Mtoto na kuendelea kuwa Balozi wa jitihada za kuboresha sekta ya afya nchini.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages