Breaking

Sunday, 8 January 2023

DKT. BITEKO AKERWA NA WAFANYABIASHARA KEMIKALI ZA KUCHENJUA MADINI KUPANDISHA BEI KIHOLELA, WATAKAOBAINIKA KUKIONA CHA MOTO



Na Samir Salum, Lango la Habari

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema wafanyabiashara wa Kemikali za kuchenjua dhahabu wanaouza kwa bei tofauti na iliyoelekezwa na Serikali watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Waziri Dkt. Biteko ameyasema hayo Januari 07, 2023 katika kikao cha wadau wanaojihusisha na uingizaji na usambazaji wa kemikali ya “Sodium Cyanide” kilichofanyika katika ukumbi wa TMDA Jijini Mwanza.

TAZAMA VIDEO HAPA CHINI
 
 Amesema kuwa amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wachimbaji wadogo kuwa kemikali ya kuchenjua madini ya dhahabu aina ya “Sodium Cyanide” inauzwa bei ya juu kwa shilingi laki nane (800,000) kwa dumu moja tofauti na bei iliyoelekezwa na serikali ambayo ni shilingi laki sita (600,000).

Amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haiko tayari kuona wachimbaji wadogo wanakwamishwa kwa hali yoyote hivyo amemuelekeza Mkemia Mkuu wa Serikali kuwafuatilia na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaouza kemikali hizo kinyume na bei elekezi.




Aidha ameshauri wafanyabiashara wa kemikali ya “Sodium Cyanide” wasio waaminifu kutopewa vibali, kuangalia upya kanuni inayotoa vibali ili kuiboresha, na kuwepo kiapo cha kibali ili yule atakayeenda kinyume achukuliwe hatua za kisheria.



Kwa upande wake Mkurugenzi wa udhibiti na usimamizi wa kemikali kutoka Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndio akizungumza kwa niaba ya Mkemia Mkuu wa Serikali amesema maelekezo yote aliyotoa Waziri Dkt. Biteko yataanza kufanyiwa kazi Mara moja.




Awali Rais wa shirikisho la vyama vya wachimbaji wadogo wa madini Tanzania (FEMATA) John Bina ameshauri Serikali kupitia Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) kuanza kuuza kemikali ya ‘Sodium Cyanide’ ambayo ni mbadala wa kemikali ya zebaki ili kuwe na mbadala inapotokea mtikisiko kutoka kwa wafanyabiashara binafsi.
 
Pia amewaasa wadau wote wa madini kushikamana na kuendelea kushirikiana na Serikali ili sekta ya madini iendelee kukua zaidi.


Mwisho.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages