Breaking

Sunday, 22 January 2023

BWENI CHUO CHA MICHEZO MALYA KUGHARIMU BILIONI 2.5



Na Shamimu Nyaki

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Januari 21, 2023 imefanya ziara katika Chuo Cha Michezo Malya kilichopo Kwimba Mwanza, kuona maendeleo ya ujenzi wa Hosteli ya Wanachuo ambayo itagharimu kiasi Cha Shilingi Bilioni 2.5 hadi kukamilika.

Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti Mhe. Stanslaus Nyongo ambaye pia ni Mbunge wa Maswa imepokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Hosteli hiyo kutoka kwa Meneja Mradi Bw. Chaguo Mghoma aliyeeleza kuwa, ujenzi wa Hosteli hiyo ni wa ghorofa nne, ambapo hatua ya kwanza itahusisha ghorofa mbili.

" Hosteli hii itakapokamilika itakua na uwezo wa kuhudumia wanachuo takriban 192 ambapo hadi Sasa umefikia asilimia 26" amesema Bw. Mghoma.

Kamati hiyo pia imetembelea eneo litakalojengwa Kituo cha Kitaifa cha kukuza na kuendeleza michezo ambacho kitahusisha Viwanja vya michezo, bwawa la kuogelea lenye hadhi ya Olimpiki, Hosteli, Jengo la Utawala, eneo la mazoezi pamoja na madarasa.

Lengo la kujenga Kituo hicho ni kuongeza wigo wa udahili wa wanachuo ili kuzalisha Wataalamu Bora wa michezo, ambapo walengwa wengi ni Wanafunzi watakaopatikana katika shule 56 zilizotengwa kwa ajili ya michezo.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul, Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Hassan Abbasi na Viongozi wengine wa wizara wameshiriki.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages