Na Lucas Raphael, Tabora
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Imetenga zaidi ya shilingi Bilioni 6.5 kwa ajili ya kuwaunganisha umeme wateja 2433 katika vitongoji 46 na kata 16 vilivyopo maeneo ya pembezoni mwa miji ya Manispaa ya Tabora na mji wa Nzega.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja uthibiti na ufuatiliaji toka wakala wa Nishati Vijijini Injinia Yusufu Ismai wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambazaa umeme katika maeneo ya pembezoni mwa miji awamu ya tatu iliyofanyika kitongoji cha Mguluko kijiji cha Itaga, kata ya Misha Manispaa ya Tabora.
Akifafanua kuhusu Mradi huo Injinia Yusufu Ismail alisema usambazaji nishati ya umeme katika maeneo yaliyo pembezoni mwa miji mkoani Tabora ndio unafika kwa mara ya kwanza.
Injinia Ismail alisema kwamba mradi huo utajenga jumla ya kilomita 48.5 za mfumo wa umeme wa msongo wa kati na kilomita 92 za msongo mdogo na watafunga mashine umba (Transfomer) 46 katika vitongoji vilivyotajwa vilivyo kwenye mradi.
Alibainsiha kwamba kampuni ya OK Electrical and Electronics Services ltd,LTD ya jijini Dar es salaam ndiyo umepewa kandarasi hiyo ya kuwaunganishia wateja wa awali 2433 ambapo aliwaomba wananchi wa maeneo utakapo pita mradi huo kuchangamkia fursa hiyo.
Aliitaja mikoa mingine ambako miradi hiyo inatekelezwa ukiachilia Tabora kuwa ni Kigoma, Geita, Tanga, Mtwara, Kagera,Singida na Mbeya.
Akizungumza wakati wa kumtambulisha Mkandarasi wa mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani amewataka wananchi wachangamkie fulsa hiyo kwa kuanza kusuka nyaya za umeme katika nyumba zao ili waweze kuunganishiwa kwa gharama ya Sh.27,000.
“Mradi huu ukikamilika unakwenda kubadilisha uchumi wa wananchi kwani watatumia umeme huo kuanzisha viwanda vidogo na shughuli zingine za uzalishaji ambazo zitawaingizia kipato na hivyo kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla” alisema Balozi Dkt. Batilda.
Mkuu huyo wa mkoa alimuomba mkandarasi wa mradi huo kampuni ya OK Electrical and Electronics Services ltd,LTD kuukamilisha ndani ya mwaka mmoja badala ya miezi 18 aliyopewa kwa sababu hakuna sababu yoyote ya kuchelewa kwa kuwa unatekelezwa kwenye maeneo yenye miundombinu mizuri.
Katika hatua nyingine Balozi Dkt Buriani amemtaka Mkandarasi kuhakikisha anatoa nafasi za ajira kwa wakazi wa maeneo husika pamoja na kuwapa malipo yao kwa wakati ili kuondoa migogoro isiyo na tija.
Naye mbunge wa jimbo la Tabora Mjini Emanuel Mwakasaka ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutekelza miradi mingi kwa mda mfupi kwa wakazi wa Tabora.
Mwakasaka alisema wataendelea kushirikiana na rais kuhakikisha miradi yote iliyoanzishwa nje na ndani ya mkoa wa Tabora inakamilika kama ilani ya chama cha mapinduzi inavyoelekeza.
Akipokea mkataba wa mradi huo Mkurugenzi wa Kampuni inayotekeleza ujenzi huo Mrisho masudi alisema lengo lake ni kutatekeleza mradi huo ndani ya mda uliopangwa na ikiwezekana chini ya mda huo.
MWISHO