Polisi katika kaunti ya Busia nchini Kenya wameanzisha msako wa kumsaka kijana mwenye umri wa miaka 22, baada ya kumkatakata baba yake wa kambo, 66, hadi kumuua kutokana na mzozo wa ardhi
Mshukiwa mtoro aliyetambuliwa kwa jina Kevin Omusolo, anadaiwa kufanya kitendo hicho cha kinyama katika kijiji cha Aciit eneo bunge la Teso Kusini , Jumamosi usiku.
Kwa mujibu wa Citizen Digital, mkuu wa polisi wa Teso Kusini, Stephen Kimunya alithibitisha kisa hicho akisema marehemu, Abisancio Opili, alikuwa na majeraha mabaya mwilini mwake baada ya kucharangwa mapanga.
Kimunya alibaini kuwa chifu wa eneo hilo alitoa ripoti ya mauaji kwa polisi, ambao walifika katika eneo la tukio.
Kimunya alisema maafisa wake waliona majeraha kwenye mwili wa marehemu, na uchunguzi ulibaini kuwa alipigana na mwanawe wa kambo kuhusu kipande cha ardhi kinachozozaniwa na Omusolo.
Mwili wa marehemu ulihamishwa hadi katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya kaunti ndogo ya Alupe ili kuhifadhiwa kabla ya uchunguzi kufanywa ili kubaini chanzo cha kifo hicho.
Chanzo: Tuko News