WATU 16 wameuawa wakati basi la abiria lilipogonga lori moja Ijumaa asubuhi Januari 6, 2023 kwenye barabara kuu ya Uganda inayounganisha mji mkuu, Kampala, na mji wa kaskazini wa Gulu.
Polisi wanasema watu 12 walifariki papo hapo huku wengine wanne wakifariki baadaye hospitalini. Wasafiri wengine kadhaa kwenye basi hilo walijeruhiwa.
Lori hilo lilisemekana kuegeshwa na kupakia mizigo takriban kilomita moja kutoka Kamdini Corner – kituo maarufu cha kusimama na ukaguzi kaskazini mwa nchi.
Kumekuwa na viwango vya kutisha vya ajali za barabarani nchini katika wiki za hivi karibuni na haswa katika msimu wa sikukuu.
Ripoti ya polisi wa trafiki mapema wiki hii ilifichua kuwa ajali 104 za barabarani zilirekodiwa kati ya 30 Desemba na 1 Januari.
Takriban watu 35 waliuawa katika ajali hizi za barabara pekee.
Ajali za barabarani zimekuwa janga la muda mrefu nchini. Polisi wa trafiki walisajili zaidi ya ajali 4,000 kote nchini Uganda mnamo 2021, nyingi zikiwa mbaya.
Via: Global Publisher