Breaking

Friday, 2 December 2022

MNF WASHAURIWA KUENDELEZA UMAJUMUI WA MWALIMU NYERERE



Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Patrobas Katambi Ameishauri Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), kuendeleza Program ya Ufadhili wa Umajumui wa Mwalimu Nyerere kwa Viongozi Vijana Afrika (Mwalimu Nyerere Pan-Africa Young Leaders Fellowship Program), ili kuzalisha viongozi wenye maadili katika nchi za Afrika.

Katambi ametoa ushauri huo wakati wa halfa ya kufunga mafunzo ya siku tano kwa vijana 60 kutoka nchi 20 za Bara la Afrika yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa kuandaliwa na MNF.

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inaunga mkono mafunzo hayo kwa kuwa yanaenda kutengeneza viongozi bora na kukuza chachu ya udugu, umoja na maendeleo katika nchi za Bara la Afrika.

“Mwalimu Julius Nyeyere alisema tumepata uhuru, lazima tufanyie kazi jukumu la maendeleo na hilo ni jambo la Waafrika wote, kwani huwezi kufanya kazi kama hauna maendeleo, utakuwa mtumwa, hivyo huu ndio msingi wa mafunzo haya ambayo yameshirikisha vijana 60,” amesema.

Naibu Waziri amesema kupitia mafunzo hayo vijana hao wameweza kujadili hatma ya nchi zao na siku wakitokea kuwa viongozi kama wabunge, mawaziri na marais watakuwa wanazungumza lugha moja kukatua changamoto zao.

Amesema kitendo cha MNF kuwafundisha vijana umajumui wa Mwalimu Nyerere kinapaswa kuungwa mkono na kila mdau kwani wanaenda kutengeneza taifa la vijana watakaosimia, amani, umoja na maendeleo ya watu.

Katambi amesema mafunzo hayo yatawezesha kuwafanya vijana ambao wanataka kuwa viongozi, kusimamia maadili na uzalendo katika nchi zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya MNF, Mzee Joseph Butiku amesema malengo ya taasisi yao ni kusimamia amani, umoja na maendeleo, hivyo program hiyo ina lengo la kujenga vijana wenye Uafrika na uongozi katika bara hilo.

Butiku amesema ili kuwa na dunia yenye amani, umoja na maendeleo ni lazima kuandaa viongozi wenye maadili, hivyo matarajio yao ni kuona program hiyo ya umajumui wa Mwalimu Nyerere inaendelezwa.

“Tumewakutanisha vijana 60 kutoka nchi 20 kwa siku tano ambapo wamefundishwa mambo mengi kuhusu uongozi, kwa kuanzia tumeona matokeo chanya na mikakati yetu ni kuhakikisha program hii inakuwa endelevu,” amesema.

Amewataka wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza kufadhili program hiyo kwa miaka mingine, ili iweze kuwa endelevu.

Ofisa Program hiyo ya Umajumui wa Mwalimu Nyerere, Joseph Malekela amesema washiriki wametoa ushirikiano wa hali ya juu, hali ambayo imewafanya wao kama waandaji kupata nguvu za kuandaa mafunzo mengine.

Malekela ametaja nchi ambazo zimetoa washiriki katika mafunzo hayo kuwa ni Tanzania Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Afrika Kusini, Ethiopia, Libya, Cameroon, Sudan, Nigeria, Sudan Kusini, Burkina Faso, Misri, Zanzibar, Botswana, Djibouti, Malawi, Zambia, Gabon na Liberia na Namibia.

Naye Balozi Noel Kaganda kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi, amewataka washiriki hao kuzingatia mafunzo ambayo wamepatiwa na kwenda kubadilisha jamii inayowazunguka.

“Naelewa mmejifunza mengi, naomba muende kusaidia jamii inayowazunguka, lakini pia zinagitie maadili, kwani huo ndio msingi wa kiongozi bora,” amesema.

Mwakilishi Mkazi wa Taasisi ya Mafunzo na Utafiti Umoja wa Mataifa (UNITAR, Svenja Voldmier amesema wataendelea kushirikiana na MNF kuhakikisha mafunzo kwa vijana viongozi yanatolewa kila mwaka.

Voldmier amesema katika kufanikisha hilo wameingia makubaliano na MNF ambayo yatachochea utekelezaji wa lengo hilo la kujenga vijana viongozi.

Kwa upande wake Jambo Ramadhani kutoka Taasisi ya Uongozi amesema kinachofanywa na MNF kinaakisi malengo yao ya kukuza viongozi ambao wanachangia maendeleo Afrika.

Mwisho.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages