WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa kote nchini wahakikishe kunakuwa na idadi ya kutosha ya mawakala wa pembejeo za kilimo katika maeneo yao ili zoezi la kufikisha mbolea kwa wakulima litekelezeke kwa ufanisi.
Amesema hayo leo (Desemba 14, 2022) alipozungumza na wakazi wa Kata ya Majimoto, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi ambako yupo kwenye ziara ya kikazi. Amewataka viongozi hao wawasimamie mawakala hao watekeleze zoezi hilo ipasavyo.
Aidha Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha shilingi bilioni 150 kama ruzuku ya ununuzi wa mbolea “Nataka niwaambie mawakala. Fedha ya ruzuku kutoka Serikalini kwa ajili ya malipo yenu ipo, pelekeni pembejeo kwa wakulima, muhimu mfanye biashara kwa weledi na uaminifu mkubwa.”
Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa Mkoa wa Katavi ambao una mawakala 10 wa kuuza pembejeo kwa wakulima umetengewa tani 4,956 za mbolea ambapo tayari tani 3,977 zimeshafikishwa mkoani humo.
Kadhalika Waziri Mkuu amewataka wakulima kuendelea kujihusisha na shughuli za kilimo hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha kwa kuwa mbolea ipo na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia amesisitiza Mkoa wa Katavi upate mbolea ya kutosha.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa muda wa wiki mbili kwa Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Filbelto Sanga na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe, Catherine Mashalla wahakikishe kituo kipya cha Afya cha Kata ya Majimoto kinaanza kutoa huduma.
Waziri Mkuu amesema kwa kuwa majengo mengi yameshakamilika likiwemo na la kutolea huduma za wagonjwa wa nje, hivyo viongozi wa Halmashauri hiyo wanatakiwa waanze kupeleka vifaa na ifikapo Desemba 27, 2022 kituo hicho kianze kutoa huduma kwa wananchi.
Ujenzi wa kituo cha Afya Majimoto ni utekelezaji wa Sera ya Serikali ya kuwa na Kituo cha Afya kwa kila Kata ili kusogeza huduma hizo karibu na makazi ya wananchi. Kituo hicho kilianza kujengwa Januari 2021 na kinatarajiwa kukamilika Februari 2023 kwa gharama ya shilingi milioni 423.8.
Vilevile, Mheshimiwa Majaliwa amewapongeza wakazi wa Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe kwa utunzaji mzuri wa mazingira hali iliyosababisha mito iliyokauka kuanza kutiririsha maji. "Endeleeni na utaratibu huu ili maji yanayoendelea kutiririka yaweze kutumika katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kilimo cha umwagiliaji.
Akitokea mkoani Katavi, Waziri Mkuu ameanza ziara ya kikazi katika Mkoa wa Rukwa ambapo ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya Sekondari ya Paramawe iliyopo Wilayani ya Nkasi. Shule hiyo inajengwa kupitia mradi wa SEQUIP.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi huo, Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo kumsimamia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ili ahakikishe anakamilisha maeneo ya ujenzi wa shule hiyo.