Breaking

Wednesday, 28 December 2022

WAZIRI MKUU AMUWAKILISHA RAIS SAMIA KUMJULIA HALI LOWASSA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Mama Regina Lowassa mke wa Waziri Mkuu Mstaafu (wa tatu kushoto) na Fredrick Lowassa (kulia) alipoenda kumjulia hali Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa anayepata matibabu jijini Johannesburg, Afrika ya Kusini, Desemba 28, 2022. Wa pili kushoto ni Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa na kushoto ni Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

*****

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwakilisha Dkt. Samia Suluhu Hassan kumjulia hali Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward Ngoyai Lowassa anayeendelea na matibabu Afrika ya Kusini.

Akizungumza na wanafamilia kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Samia, Waziri Mkuu amewasilisha salaam za pole kutoka kwa Mheshimiwa Rais na kusema Mheshimiwa Rais anafuatilia hali ya Mheshimiwa Lowassa kwa ukaribu na anamuombea afya njema.


Waziri Mkuu ametoa salamu hizo leo Jumatano, Desemba 28, 2022 jijini Johannesburg, Afrika Kusini ambako alienda kumjulia hali Mheshimiwa Lowassa.


Kwa upande wake, Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu, Mama Regina Lowassa amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo amekuwa karibu na wanafamilia na namna ambavyo anafuatilia matibabu ya mpendwa wao.


Naye mtoto mkubwa wa Mheshimiwa Lowassa na Mbunge wa Monduli, Bw. Fredrick Lowassa amewashukuru Watanzania kwa maombi yao ya kumtakia afya njema baba yao.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages