Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio la wizi wa mtoto mchanga mwenye umri wa mwezi mmoja aliyepotea katika mtaa wa Migera kata ya Nshambya Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.
Akizungumza na vyombo vya habari mapema leo ofisini kwake Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Kagera ACP William Mwampaghale amesema kuwa mtoto huyo aliyejulikana kwa majina ya Benita Beneti amepotea Desemba mosi 2022 majira ya saa tatu na nusu usiku ambapo mama wa mtoto huyo aliyejulikana kwa majina ya Johanitha Augustino aligundua kuibiwa kwa mtoto wake huyo aliyemuacha kitandani akiwa amelala ndani ya nyumba yao.
ACP Mwampaghale ameeleza kuwa mnamo tarehe hiyo mama wa mtoto huyo alipata wageni watatu ambao aliishi nao katika mtaa wa Omukigusha Manispaa ya Bukoba kwa lengo la kumsalimia na mara baada ya kumsalimia waliaga na kuondoka.
Na kwamba majira ya saa tatu na nusu usiku walirudi tena wakiwa wawili na kumtaka wazungumze naye lakini mama huyo alikataa na kuwa ahidi kuzungumza nao tarehe 02 Desemba 2022, majira ya mchana Kisha wakamtaka mama huyo awasindikize na mara baada ya kuwasindikiza alirudi chumbani kwake na kubaini kupotea kwa mtoto wake aliyemuacha kitandani.
Aidha Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi watakao ona mtoto ambaye wanahisi yupo na mtu au watu ambao sio wake kutoa taarifa haraka kwa Jeshi la Polisi ili hatua zichukuliwe na kwamba ikiwa ni siku 16 za maadhimisho ya kupinga ukatili wa kijinsia ikiwa kauli mbiu ni "Kila uhai una thamani tokomeza mauaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto" hivyo wananchi wote waipokee na kuhakikisha wanatokomeza vitendo vyote vya ukatili ikiwemo kuibiwa na kutelekezwa.
Via: Malunde 1 Blog