Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amewataka wamiliki wa leseni za madini nchini kuchangia huduma kwa jamii inayozunguka mgodi ambapo amesema Sheria ya Madini Sura 123 inaeleza wazi kuhusu wajibu wa wamiliki wa leseni kwa jamii.
Dkt. Biteko amesema hayo baada ya kutembelea mgodi wa Sinai Gold Mine uliopo katika kijiji cha Ugenzi kata ya Sinai wilayani Mufindi mkoa wa Iringa.
Aidha, Dkt. Biteko ameagiza mialo yote katika mgodi wa Sinai kusajiliwa na kutafutiwa eneo moja ambalo mialo hiyo itajengwa kwa lengo la kuimarisha usimamizi na kudhibiti utoroshaji wa madini.
"Hapa kuna mialo imesambaa katika maeneo tofauti, niwaombe Ofisi ya Afisa Madini kusajili mialo yote iliyopo katika eneo hili na muitafutie eneo moja ili tujue mwalo gani imezalisha kiasi na pia wenye mialo mnatakiwa kutunza kumbukumbu za uzalishaji wenu," amesema Dkt. Biteko.
Pia, Dkt. Biteko amesisitiza kila mchimbaji wa madini kuwa mlinzi wa mwenzake na kuona wivu wa maendeleo kwa Taifa lao ili kukomesha vitendo vya utoroshaji wa madini.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Saad Mutambule amempongeza Dkt. Biteko kwa kufanya ziara wilayani humo na kumuomba kufanyike tafiti za madini katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo ili wachimbaji wadogo wa madini waondokane na uchimbaji wa kubahatisha.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Iringa, Abdulrahman Milandu ametoa wito kwa wawekezaji kote nchini kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya Madini mkoani Iringa ambapo amesema mkoa huo umebalikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali ikiwemo dhahabu, vito, madini ya viwandani na madini ya ujenzi.