Breaking

Thursday, 15 December 2022

WAAJIRI WATAKIWA KUTATUA CHANGAMOTO YA UHABA WA WATUMISHI KUZIBA NAFASI KADA ZENYE UHITAJI



Na. Veronica E. Mwafisi-Kigamboni

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka waajiri katika Taasisi za Umma kuhakikisha wanatatua changamoto ya upungufu wa watumishi katika baadhi ya kada kwa kuwabaini watumishi wenye ujuzi wa kada hizo na kuwaendeleza kielimu ili wapate sifa ya kuziba nafasi wazi na hatimaye kutatua changamoto hiyo ya uhaba wa watumishi, badala ya kuisubiri Serikali kutatua changamoto hiyo.

Akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni Disemba 14, 2022 Mhe. Ndejembi amesema, waajiri wanapaswa kubaini watumishi wenye ujuzi na sifa ili kuwajengea uwezo kiutendaji kupitia programu za mafunzo kwani watakapohitimu watarejea katika vituo vyao vya kazi wakiwa na ujuzi na elimu itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, Serikali inaajiri watumishi kulingana na bajeti iliyopangwa katika mwaka wa fedha husika, kwa mantiki hiyo, bajeti inaweza kutokidhi kuajiri watumishi kulingana na uhitaji, hivyo waajiri wanayo nafasi ya kuisaidia Serikali kutatua changamoto ya uhaba wa watumishi kwa kuwaendeleza baadhi ya watumishi watakaosaidia kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi kwenye kada zenye uhitaji.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka waajiri kutowakaimisha nafasi watumishi wasio na sifa na utaalamu wa kazi katika kada wanazotakiwa kuzisimamia, na kuongeza kuwa ni muhimu kwa watumishi wanaokaimishwa kuwa na sifa na uwezo utakaowasaidia kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Bw. Erasto Kiwale amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kufanya ziara ya kikazi katika halmashauri hiyo na kuhimiza uwajibikaji, kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi, kutatua kero pamoja na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili watumishi wa halmashauri yake.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi anaendelea na ziara yake ya kikazi jijini Dar es salaam yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).





Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages