Breaking

Thursday, 29 December 2022

TPAWU WALIA NYONGEZA YA MISHAHARA



Na Selemani Msuya

CHAMA cha Wafanyakazi Mashambani na Kilimo Tanzania (TPAWU), kimesema Sh.40,000 iliyoongezwa kwenye kima cha chini cha mshahara wa mfanyakazi wa sekta ya kilimo haikiwezi kukidhi mahitaji yao.

Taarifa ya kutokubaliana na kiwango hicho cha nyongeza ya mshahara imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa TPAWU Taifa, Fred Akondowe wakati akizungumza na waandishi wa habari.

“Tunatoa maoni yetu juu ya Tangazo la Serikali namba 45/2022 kama ifuatavyo, kiwango cha mshahara kilichoongezwa ni kidogo mno kiasi cha kutomwezesha mfanyakazi kumudu mahitaji yake ya kila siku, Serikali kupitia bodi ya kima cha chini cha mshahara imeongeza Sh. 40,000 kwa sekta ya kilimo kutoka kwenye kima cha chini cha mshahara cha mwaka 2013 baada ya miaka 9 kupita na kufanya kima cha chini cha mshahara kwa mfanyakazi wa sekta ya kilimo kuwa ni Sh. 140,000.


“Jambo hili haliko sawa kabisa, Serikali ituambie ni kwa namna gani mfanyakazi anaweza kumudu maisha yake kwa Sh.140,000 kwa mwezi ikiwa ni pamoja na malazi, makazi, chakula, elimu na afya,” amesema Akondowe.

Aidha, mwenyekiti huyo amesema nyongeza hiyo ya Sh.40,000 inawafanya wafanyakazi wa sekta ya kilimo kukosa huduma ya bima ya afya inayotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kuwa mshahara hautimizi vigezo na masharti ya mfuko huo.

“Kiwango cha chini cha kuchangia NHIF ni kuanzia Sh.40,000 ikiwa ni asilimia 6 ya mshahara wa mfanyakazi ambapo mfanyakazi anaweza kuchangia kutoka kwenye mshahara wake silimia 3 na mwajiri asilimia 3 hivyo kwa wafanyakazi wa sekta ya kilimo asilimia 3 inayotakiwa kuchangiwa ni Sh.20,000 wakati wao katika mshahara wao wa Sh. 140,000 na asilimia 3 ni Sh. 4,200 ambapo pia mwajiri akimchangia asilimia 3 hiyo hiyo inakuwa Sh. 8,400 fedha ambayo ni ndogo kiasi cha kutokidhi kiwango cha chini cha kuwa mwanachama wa NHIF ambacho ni Sh. 40,000.

Akondowe amesema wafanyakazi wengi wa sekta ya kilimo kwa kupitia mikataba ya hali bora za kazi wanalipwa kati ya Sh.162,000 na Sh. 400,000 kama kima cha chini cha mshahara, mfano Sekta ya Chai kima cha chini Sh. 175,532/, Mkonge Sh.161,928, Miwa Sh.278,684, Maua Sh.304,390, Misitu Sh. 215,000, Mazao Mchanganyiko Sh. 200,307.

Mwenyekiti huyo amesema pamoja na kamati ya kima cha chini cha mshahara kuhoji viwango vya mishahara vinavyolipika kwa sasa katika sekta ya kilimo na TPAWU kuwaonesha hali halisi kwa kuwapatia nakala za mikataba ya hali bora za kazi, wanashangaa kuona bodi imependekeza kiwango cha Sh. 140,000.

“TPAWU tunasema nyogeza hii haitaleta maboresho ya aina yoyote kwa wafanyakazi wa sekta ya kilimo mbali na kushusha motisha ya utendaji kazi,”amesema.

“Katika tangazo namba 45/2022, Serikali imetangaza na viwango tofauti kwa sekta tatu ambapo katika tangazo la Serikali Nambari 196 la 2013 sekta hizo zilikuwa na kiwango kimoja ambazo ni kilimo, ulinzi makampuni madogo na viwanda, zote zilikuwa na kiwango cha Sh.100,000, lakini katika GN 45 ya 2022 Serikali imepanga viwango tofauti vya malipo katika sekta hizo, kilimo Sh. 140,000, ulinzi makampuni madogo Sh. 148,000 na viwanda Sh. 150,000.

Swali la kawaida kamati ya wataalam pamoja na wajumbe wa bodi walifanya utafiti upi ili kuja na viwango hivyo tofauti na kile kilichofanyiwa utafiti 2013? Ubaguzi huu wa wazi kwa wafanyakazi haukubaliki,” amesema.

Akondowe amesema vyama vya wafanyakazi kupitia TUCTA vilijulishwa kuwa kutokana na umuhimu na uharaka wa kupatikana kima cha chini cha mshahara sekta binafsi, kima cha chini cha mshahara kitakachotangazwa kitaanza kutumika July 2022 na kitakuwa cha mpito, lakini kwenye tangazo imetangazwa kuwa kima cha chini cha mshahara kitaanza kutumika Januari 2023 na hawaoni kama kima hicho ni cha mpito.

Amesema kama kima hicho sio cha mpito basi utaratibu wa kisheria haukufuatwa na hivyo viwango vilivyopendekezwa ni vya kufikirika, havina ushahidi wa kitafiti, hivyo wanaitaka Serikali irudie kufanya mchakato ikiwemo utafiti na hatua zingine za kisheria zitakazopelekea kupatikana kwa kima cha chini cha mshahara kilichofuata utaratibu wa kisheria.



Mwisho
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages