Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 21 Disemba, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Programu ya TAKUKURU RAFIKI aliyoizindua inatoa fursa kwa kila Mtanzania kushirikiana na Serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika kutekeleza jukumu la kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa ambavyo ni kikwazo kikubwa cha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dodoma, wakati akizindua Programu ya TAKUKURU RAFIKI kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) uliofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa St. Gasper.
Mhe. Jenista amesema kuwa, kupitia TAKUKURU RAFIKI kila Mtanzania atajiona kuwa ni sehemu ya TAKUKURU na anao wajibu wa kuzuia vitendo vya rushwa mahali alipo, anapoishi, anapofanya biashara au kazi yoyote ambayo inaendesha maisha yake.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa TAKUKURU kupitia programu ya TAKUKURU RAFIKI itajiweka karibu na jamii na kuwa rafiki wa wananchi hivyo, kuwawezesha wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa urahisi ambazo zitaiwezesha TAKUKURU kutekeleza wajibu wake kwa manufaa ya taifa.
“Leo nimezindua TAKUKURU RAFIKI ambayo faida yake kwa taifa ni kuboresha mifumo ya utoaji wa taarifa na elimu kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, ili kila mwananchi ashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa nchini,” Mhe. Jenista amefafanua.
Mhe. Jenista amesisitiza kuwa, programu ya TAKUKURU RAFIKI itajenga utayari wa wananchi kuichukia rushwa na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa ni adui mkubwa wa maendeleo katika taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, ACP Salum Hamduni amesema TAKUKURU RAFIKI ni programu ambayo itaongeza wigo wa wananchi kushiriki katika utambuzi na utatuzi wa vitendo vya rushwa katika jamii na kuongeza kuwa, katika kutekeleza programu hiyo taasisi yake itajielekeza zaidi kwenye usimamizi wa utoaji wa huduma za kijamii na fedha zilizotolewa na Serikali kutekeleza miradi katika sekta za kipaumbele za maji, elimu, kilimo, afya, barabara na ardhi.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo amesema kuwa Programu ya TAKUKURU RAFIKI itamuwezesha mwananchi kutambua thamani ya mradi unaotekelezwa katika eneo alilopo na ni kwa namna gani atashiriki katika kusimamia utekelezaji wake ili uwe na tija katika jamii.
Programu ya TAKUKURU RAFIKI imezinduliwa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU ambao kaulimbiu yake ni ‘Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu: Tutimize Wajibu Wetu’.