Breaking

Monday, 19 December 2022

POLISI SHINYANGA WAKAMATA VITU VYA WIZI, WABAKAJI WACHAPWA VIBOKO



JESHI la Polisi mkoani Shinyanga, limekamata vitu mbalimbali vya wizi, pamoja na bunduki na madawa ya kulevya, huku likieleza kuwatia mbaroni baadhi ya watuhumiwa wakiwamo na wabakaji kuhukumiwa kuchapwa viboko na kufungwa jela.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi, amebainisha hayo leo Desemba 19, 2022, wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya msako ambao wameufanya kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Novemba 22 hadi Desemba 12 mwaka huu.

Amesema katika msako huo wamekamata vifaa tiba vya zahanati ya Uyongo halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, Bunduki moja aina ya Gobore, simu za mkononi 17, Pikipiki 10, dawa za kulevya Heroine 10, Bangi kete 71, Tv Nne, Mitungi ya Gesi miwili na lita 20 za Gongo.

Ametaja vitu vingine ambavyo wamevikamata kuwa ni vyuma vya ujenzi wa minara ya TANESCO, Spika Mbili, vitenge doti Nne, Kopyuta tatu, Subwoofer Nne, Monita moja, Godoro moja, panga moja, shoka moja, makabati mawili ya kuhifadhia Chips, huku wakiokota Pikipiki Nane na Baiskeli 11.

“Tunawaomba wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wafike katika kituo kikubwa cha Polisi Shinyanga mjini kwa ajili ya kuzitambua mali zao kuanzia tarehe 22 hadi 30 mwezi huu,”amesema Magomi.

Aidha, amesema katika kipindi hicho wamefanikiwa kuwafikisha watuhumiwa mahakamani na kutolewa hukumu mbalimbali, wakiwamo wabakaji kuchapwa viboko na kufungwa Jela wakiwamo na watu waliojihusisha na vitendo vya ulawiti, kujeruhi, wizi wa mtoto na kumpa mimba mwanafunzi.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages