Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Bw.Christopher Mramba, ameitaka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kuwafuatilia kwa karibu wale wote wanaorasimisha biashara ili kujiridhisha kama wanafanya biashara zilizokusudiwa.
Bw. Mramba ametoa wito huo alipotembelea banda la BRELA katika Maonesho ya Bidhaa za Viwanda yaliyohitimishwa tarehe 09 Disemba, 2022 kwenye Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Nyerere (Sabasaba), Jijini Dar es salaam.
Amesema amekuwa akipokea malalamiko kuhusu baadhi ya wafanyabiashara kutofanya kazi kulingana na vyeti vya usajili pamoja na leseni za biashara walizopewa, hivyo ni vyema BRELA ikaangalia jinsi ya kuwafuatilia, ili kuepuka utapeli.
Bw. Mramba alimuwakilisha Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), na maonesho hayo yalifungwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, (TanTrade), Prof. Ulingeta Mbamba.