Breaking

Tuesday, 13 December 2022

LIKIZO KWA WATUMISHI WA UMMA NYAKATI ZA SIKUKUU ZISIWE KIKWAZO CHA KUWAHUDUMIA WANANCHI



Na. Veronica E. Mwafisi-Kinondoni

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema likizo za mwaka kwa watumishi wa umma katika kipindi cha sikukuu zisiwe kikwazo cha kutoa huduma kwa wananchi.

Akizungumza na Watumishi wa Umma wa Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, leo jumanne Disemba 13, 2022 Mhe. Ndejembi amesema, likizo ya mwaka ni haki ya mtumishi lakini inatakiwa kuchukuliwa kwa tahadhari hasa katika kipindi cha sikukuu ili isiathiri utoaji wa huduma kwa wananchi wanaofuata huduma katika taasisi za Serikali.

Mhe. Ndejembi amesema watumishi wanapochukua likizo kipindi cha sikukuu, ni vema baadhi wakabaki ofisini ili kuendelea kutoa huduma kama kawaida kwani wananchi wanahitaji huduma nyakati zote za sikukuu na za kawaida.

“Tuhakikishe huduma zinatolewa kama kawaida katika vituo vyetu vya kazi katika kipindi hiki cha Sikukuu kama zinavyotolewa katika siku za kawaida kwani serikali hailali, hufanya kazi wakati wote,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka watumishi wa umma nchini kujitathmini kiutendaji kwa kujiwekea malengo kupitia watumishi binafsi, Idara na Taasisi kwa ujumla katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi ili kuunga mkono kwa vitendo Kaulimbiu ya Kazi Iendelee ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Bi. Stella Msofe amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuhimiza uwajibikaji, kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwa ni pamoja na kutatua kero na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili watumishi walio katika wilaya yake.

Bi. Msofe, ameahidi kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Naibu Waziri aliyoyatoa kwa watumishi kwa kushirikiana na wasaidizi wake kuanzia ngazi ya Kata, Mtaa na Halmashauri kwa ujumla.

Naye, Mtumishi wa Manispaa ya Kinondoni, Bi. Happyfania Mabala amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi, ikiwa ni pamoja na kutatua kero na changamoto zilizokuwa zikiwakabili watumishi wa Halmashauri hiyo kwa muda mrefu.

Kadhalika, Bi. Mabala ameushukuru uongozi wa Wilaya yake kwa kuwakaribisha viongozi mbalimbali na kuzungumza nao masuala ya kiutumishi, jambo ambalo linawaongezea ari kubwa katika utendaji kazi wao kupitia utumishi wa umma.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameanza ziara ya kikazi jijini Dar es salaam yenye lengo kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages