Breaking

Monday, 19 December 2022

INDIA YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA UONGEZAJI THAMANI MADINI



Serikali ya India imeahidi kushirikiana na Tanzania katika uendelezaji wa teknolojia za uongezaji thamani madini nchini kupitia Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC).

Hayo yamebainishwa na Waziri anayeshughulikia Migodi nchini India Mhe. Pralhad Joshi wakati wa ziara ya Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko katika ofisi za Waziri hiyo ndani ya Bunge nchini India.

Waziri wa India Mhe.Josh amesema Serikali ya India imeonesha nia ya kuwekeza nchini katika madini ya Kimkakati na makaa ya mawe.

Kutokana na uwepo wa fursa hizo Dkt. Biteko na Waziri wa India wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika Sekta ya Madini kati ya Tanzania na India.

Pia, aliahidi kuendeleza ushirikiano kupitia Wizara ya Biashara ya nchini India na Baraza la kukuza usafirishaji Vito na bidhaa za usonara ( Gem and Jewellery Export Promotion Council).

Katika hatua nyingine, Waziri wa Madini Dkt. Biteko alikutana na Kampuni ya Cancastmaxx katika ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini India ambayo imeonesha nia ya kuwekeza katika makaa ya mawe nchini kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Dkt. Biteko aliiagiza kampuni hiyo kufuata taratibu na kujiridhisha ili kutimiza azma ya kuwekeza Tanzania.

Pia, Dkt. Biteko alikutana na na wadau wa Baraza la kukuza Usafishaji Vito na bidhaa za usonara kwa lengo la kubadilishana uzoefu kwenye tasnia ya uongezaji thamani madini na kutangaza fursa zilizopo katika tasnia ya madini.

Wadau hao walikubali kushurikiana katika kuboresha tasnia ya uongezaji thamani madini nchini kupitia Kituo cha TGC na kukuza masoko ya madini ya vito.

Dkt. Biteko alitembelea Kiwanda cha kukata na nlkung'arisha madini ya vito na utengenezaji wa bidhaa za usonara ambapo alishuhudia ukataji wa madini ya vito na utengenezaji wa bidhaa za usonara zenye ubora wa kiwango cha juu.

Katika ziara hiyo, Dkt. Biteko aliambatana na Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga, Mwenyekiti wa Bodi ya TGC Dkt. George Mofulu na Mratibu wa TGC Daniel Kidesheni na wakufunzi kutoka kituo hicho Jumanne Shimba, Ester Njiwa na Cleophas Siame.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages