Na. Veronica Mwafisi – Dar es salaam
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutoa kipaumbele cha kuwapatia mikopo walengwa wa TASAF walio kwenye vikundi, kupitia fedha za asilimia 10 zinazotengwa kwa ajili ya kuvikopesha vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu ili mikopo hiyo iboreshe maisha ya kaya maskini nchini kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekusudia.
Mhe. Ndejembi ametoa rai hiyo Disemba 17, 2022, kwa Wakurugenzi wa Halmashauri nchini wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mhe. Ndejembi amesema, ameweza kutembelea vikundi mbalimbali vya walengwa wa TASAF katika Halmashauri zote zilizopo jijini Dar es salaam na kuona utekelezaji wa kazi za vikundi mbalimbali vinavyojumuisha Vijana, Wazee, Walemavu na Wanawake.
“Wilayani Kinondoni kuna vijana walio kwenye vikundi vya TASAF walipatiwa mikopo wa pikipiki ambapo wamemudu kurejesha, pia wanawake Temeke walio kwenye vikundi vya TASAF wamepatiwa mikopo ya shilingi milioni 10 na Ilala wamepatiwa milioni 30 ambayo imewawezesha kuboresha maisha yao na kujishughulisha na ujasiliamali,”Mhe. Ndejembi amefafanua.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Bi. Salome Mwakigomba amesema TASAF imefanya jitihada kubwakuhamasisha uundaji wavikundi vya walengwa katika halmashauri zote ambazo Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unatekelezwa hivyo wakipatiwa mikopo hiyo ya asilimia 10 watendelea kuboresha maisha yao.
Bi. Mwakigomba amesema, TASAF itatekeleza maelekezo ya Ndejembi ya kuwahamasisha walengwa wa TASAF kuwa na miradi endelevu ili wajiongezee kipato kitakachowawezesha kuboresha maisha yao.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara yake ya kikazi Mkoani Dar es salaam iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).