Waendesha bodaboda wa Nakuru nchini Kenya wamemwogesha mwenzao na kumnunulia chupi baada ya wateja kulalamikia uvondo mkali wa mwili wake.
Waendeshaji hao wa bodaboda kutoka Molo waliwapoteza wateja kwa siku nyingi ambao walilalamikia usafi wao na hivyo kuamua kuchunguza kati yao ni nani ambaye hakuwa akioga.
Wakizungumza na Inooro TV, waendeshaji hao walisema walikwenda mtoni kumwogesha baada ya kubaini kuwa ni muda mrefu tangu aoge.
Walichanga pesa kati yao ili kumnunulia mwenzao sabuni na vitu vingine.
"Wateja walikuwa wamelalamika kwa muda mrefu kwamba sisi ni wachafu. Walipoacha kuja kwetu, ilibidi tujue ni nani kati yetu ambaye hakuwa akioga," mmoja wa waendeshaji bodaboda alisema.
“Tunashangaa kwa sababu tukiwa mtoni tukimwogesha tuligundua hana hata nguo za ndani na tumemnunulia mpya,” mhudumu mwingine wa bodaboda alibainisha.
Baada ya mwili wake wote kupakwa sabuni, na kuchanwa na wenzake, bodaboda huyo alitoka nje ya mto akiwa amezaliwa upya.
“Nko freshi barida,” alisema.