Karagwe - Kagera
Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa Madiwani wote katika halmashauri ya Wilaya Karagwe kuendelea kusimamia kikamilifu fedha za miradi ya Maendeleo inayotekelezwa katika Kata zao ili iweze kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wanaowawakilisha.
Bashungwa ametoa wito huo Desemba 23, 2022 wakati alipokutana na Madiwani wote wa Halmashauri ya wilaya Karagwe kwa ajili ya kupeana mrejesho wa masuala yote yaliyotekelezwa katika mwaka 2022 na kujipanga kwa mwaka 2023.
Bashungwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepeleka fedha nyingi za maendeleo katika maeneo yote nchini ili kutekeleza miradi mbalimbali inayohitaji usimamazi wa karibu hass katika ngazi za chini.
Aidha, Amewapongeza Madiwani kwa kazi kubwa ya wanaoendelea kufanya katika kata zote ambayo inawafanya wananchi waendelee kuwa na imani kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi.
Bashungwa ameeleza mataminio yake ni kuendelea kuona kila Diwani anakuwa karibu na wananchi na kusikiliza kero zinazojitokeza ili ziweze kupatiwa ufumbuzi mapema iwezekanavyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri na Diwani kata Nyaishozi, Wallace Mashanda ameeleza kuwa katika Mwaka 2023, Halmashauri itajikita kuimarisha ukusanyaji wa mapato na usimamizi madhubuti wa fedha za miradi ya maendeleo.
Vile vile, Mashanda ameeleza mkazo mkubwa pia utawekwa katika kuimarisha Utendaji wa Watumishi wa ngazi zote na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi bila usumbufu na kuziba mianya ya rushwa.
Nae, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Karagwe, Paschal Rwamugata amesema Chama Cha Mapinduzi kinarudhishwa na kasi ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kata na amewataka madiwani kuongeza nguvu katika Usimamizi wa masuala yote yanayoendelea kutekelezwa katika Kata zao.