Breaking

Friday, 30 December 2022

BANDARI TANGA KUPOKEA TANI MILIONI 3, KUKUZA UCHUMI, AJIRA



Na Selemani Msuya

MAMLAKA ya Bandari ya Tanga imesema maboresho ya bandari hiyo yatawezesha kupokea zaidi ya tani milioni 3 za shehena za mizigo kwa mwaka, kutoka tani 750,000, hali ambayo itachochea ukuaji wa uchumi wa nchi na wananchi.


Hayo yamesemwa na Meneja wa Bandari hiyo, Masoud Mrisha wakati akizungumza na waandishi wa habari za uchumi, biashara na uwekezaji waliotembelea bandari Disemba 28, 2022.


Mrisha amesema Agosti 2019 Serikali iliagiza kufanyika kwa maboresho ya bandari hiyo ambapo hadi yatakapokamilika Aprili 2023 jumla ya Sh.bilioni 429.1 zitatumika.


Amesema maboresho ya bandari hiyo yatawezesha utoaji huduma kwa meli kubwa ambazo awali zilikuwa hazifiki hapo, hivyo kusababisha gharama kubwa


"Zaidi Sh.bilioni 429 zimetumika kufanya maboresho Bandari ya Tanga, matarajio yetu ni baada ya kukamilika tutaweza kupokea mzigo mwingi hadi kufikia tani milioni 3 kutoka tani laki 750,000," amesema.


Amesema pamoja na kuongeza uwezo wa kupokea mzigo, pia mapato yataongezeka na uchumi wa Tanga, mikoa ya Kaskazini na nchi kwa ujumla utakuwa.


Mrisha amesema pia maboresho hayo yatawezesha ajira kuongezeka.


“Gharama za Mradi huu kwa awamu ya kwanza ulikuwa Sh.bilioni 172.4,″ amesema Mrisha.


Mrisha amesema maboresho hayo yamehusiha uongezaji wa kina cha maji kutoka mita tatu hadi mita 13 na upana wa mita 73 kwenye njia ya kuingiza na kutokea meli, ambapo awali mzigo ulikuwa unafutwa umbali wa kilomita 1.7 kutoka kwenye gati.


Meneja huyo amesema kwa sasa wapo katika awamu ya pili ya maboresho ya bandari ya Tanga yaliyoanza Septemba 2020 na hadi sasa yamefikia asilimia 83, yanatarajiwa kukamilika Aprili 2023 ambapo takribani bilioni 256.8 zitatumika.


Amesema awamu hiyo ya pili ya mradi imehusisha maboresho ya magati mawili yenye urefu wa mita 450.


Mrisho amesema maboresho, gati hizo mbili za Bandari ya Tanga zilizojengwa mwaka 1914 na 1954, zimeongezwa kwa mita 50 upande wa Mashariki na mita 92 upande wa Magharibi kuelekea baaharini.


Mrisha amesema
Bandari ya Tanga ni fursa kwa wafanyabiashara wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara pamoja na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.


"Kuanzia Aprili mwaka 2023 tutaanza kupokea meli kubwa mbili za mizigo na mbili za mafuta hivyo tunawaomba Watanzania kutumia bandari hii, inafikika kirahisi,"amesema.


Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ongezeko la shehena katika bandari ya Tanga limekuwa kwa wastani wa asilimia 20 kutoka shehena tani 502,426 mwaka 2017/18 hadi kufikia tani 986,308 mwaka 2021/22 kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa na bandari hiyo.


Meneja huyo amesema Bandari ya Tanga imetoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 254 ambapo kati yao, 199 ni wanaume na wanawake ni 55 tu sawa na asilimia 22.


Katika mradi wa maboresho bandari ya Tanga pia inapanua wigo wa sehemu ya kuhifadhia makontena kutoka uwezo wa kuhifadhi makontena 1,000 hadi kufikia uwezo wa kuhifadhi makontena 12,000.


Ofisa Masoko Bandari ya Tanga, Rose Tandiko amesema uli uwekezaji huo uwe na tija katika mkoa na Tiafa, serikali inapaswa kushauri na kuelekezwa wafanyabiashara wa mikoa ya karibu na bandari kutumia bandari hiyo.


"Huu uwekezaji ni mkubwa sana, ili uwe na tija, tunaomba wawekezaji na wasafirishaji hasa wa Ukanda wa Kaskazini kutumia bandari hii. Ni imani yetu Serikali itaweka mkazo," amesema Tandiko.


Amesema mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na kwingineko inapaswa kutumia bandari hiyo kwani gharama zake sio kubwa.


Tandiko amesema mazao ya Kahawa, Mkonge na mengine yanapaswa kusafirishwa kupitia bandari ya Tanga.


Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema amewataka wananchi wa Tanga na maeneo mengine kuwekeza Tanga ili waweze kunufaika na bandari hiyo ya kisasa.


Mnyema amesema faida zimeanza kuonekana katika mradi wa maboresho ya bandari ya Tanga yanayoendelea kwani hivi sasa nchi jirani zimeanza kutumia bandari hiyo.


“Faida ambazo zimeanza kupatikana ni pamoja na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Rwanda na Burundi kuanza kuitumia bandari yetu ya Tanga kwa sababu inakuwa rahisi tofauti na sehemu nyingine” amesema Mnyema.


Meya wa jiji la Tanga Abdulrahman Shiloow amesema kukamilika kwa maboresho hayo yanaenda kuleta mapinduzi ya kiuchumi mkoani humo.


Shiloow amesema ni wakati muafaka kwa wawekezaji kuwekeza Tanga, ili kuweza kuirejesha Tanga ya zamani.


"Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu fedha za mradi huu, naamini kilichobakia ni sisi wana Tanga na mikoa jirani kunufaika,"amesema.


Naye Mwanahamis Msemo amesema maboresho hayo yamekuwa neema kwake, kwani ameweza amepata kipato na kusomesha watoto wake na kupata mahitaji mengine.


Amesema kupitia kazi ambazo anafanya bandarini hapo, ameonesha wanawake wenzake kuwa wanawake wanaweza na sio lazima wawe tegemezi.

“Nimepata kazi hii, imenisaidia mimi na familia yangu, nashukuru sana Bandari Tanga, wanawake tusichagu kazi," amesema.



Mwisho


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages