Breaking

Sunday, 25 December 2022

ASKOFU SANGU AHUBIRI AMANI, AKEMEA UKATILI SALAMU ZA KRISMASI NA MWAKA MPYA 2023


Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, ametuma salaam za Krismas na mwaka mpya wa 2023, kwa Waamini na watu wote, huku akisisitiza Watanzania kuendelea kumwombea rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na wandamizi wake, ili waliongoze taifa kwa amani, umoja na mshikamano.

Amewasihi Watanzania kuepuka kushiriki mambo yote ambayo yanaweza kuvuruga amani ya nchi, na pale wanapokuwa na jambo la kuwashauri viongozi wao wafanye hivyo kwa hekima na upendo, kwa kuzingatia zaidi maslahi mapana ya taifa.

“Twatambua kuwa mkamilifu ni Mungu peke yake , hivyo Tunapokuwa na jambo la kuwashauri viongozi wetu, tufanye hivyo kwa hekima na upendo huku tukiacha ubinafsi na kuzingatia zaidi maslahi mapana ya taifa letu“

Askofu Sangu amewataka wale waliopewa dhamana ya kuwaongoza wananchi, kutekeleza wajibu wao kwa uaminifu na uadilifu kwa manufaa ya wote, na siyo kwa kuangalia maslahi yao binafsi.

Halikadhalika, amesisitiza suala la kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji, ili kuepuka mabadiloko hasi ya tabianchi ambayo yanaathiri kwa kiasi kikubwa hali ya hewa na kwamba, kuharibu mazingira ni kuharibu kazi njema ya uumbaji iliyofanywa na mwenyezi Mungu na kuua kizazi kijacho.

Askofu Sangu pia amezungumzia suala ya ukatili kwa wanawake na watoto na kubainisha kuwa, pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau kudhibiti hali hiyo, bado kila Mtanzania anao wajibu wa kuwa balozi katika kukabiliana na vitendo hivyo ambavyo vina athari kubwa za muda mfupi na muda mrefu kwa ustawi wa jamii .

Amewaomba vingozi wote wa dini kuendelea kutumia nyumba za ibada kuwaelimisha Waamini ili wawe mabalozi wa kupinga vitendo hivyo, ikiwemo mila na tamaduni zote zinazochangia kuendelea kwa ukatili huo.

“Sisi viongozi wa dini tuendelee kutumia nyumba zetu za ibada kuwaelimisha waamini wetu ili wawe mabalozi wa kupinga hali hiyo ikiwemo mila na tamaduni zote zinazochangia kuendelea kwa ukatili huo“

Soma zaidi >>HAPA<<

Via: Radio Faraja Fm
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages