JESHI la Polisi Mkoa wa Kagera limefanikiwa kuzuia tukio la ujambazi wa kutumia silaha lililokuwa linapangwa na majambazi watatu waliokuwa wanajaribu kuvamia kituo cha mafuta (petrol station) cha Benaco Oil kilichopo Benako Wilaya ya Ngara mkoani humo.
Kamanda wa polisi mkoani Kagera William Mwampaghale amesema kuwa Desemba 07 mwaka huu askari polisi wakiwa katika doria walipata taarifa fiche kuwa kuna watu wanajiandaa kufanya uhalifu wa kutumia silaha katika kituo hicho cha mafuta, na kuweka mtego wa kuwanasa.
Kamanda huyo amesema kuwa ilipofika saa 5:30 usiku, askari polisi wakiwa katika maficho waliwaona watu watatu na kuwaamrisha wasimame na kwamba baada ya watu hao kugundua kuwa wanasimamishwa na askari walianza kurusha risasi ovyo kuelekea walipokuwa askari, hali iliyosababisha askari hao kujibu na kumjeruhi mtu huyo aliyepoteza maisha wakati akiwahishwa hospitali.
"Askari hao walifanikiwa kumjeruhi mmoja, mmoja alitoroka na mwingine alijisalimisha, tulifanya upekuzi na kupata bunduki moja aina ya AK 47 na magazine tatu zikiwa na jumla ya risasi 25, aliyejisalimisha tunaendelea kumhoji ili kupata taarifa zaidi juu ya aliyetoroka lakini pia kujua wengine wanaoshirikiana nao kufanya uhalifu" amesema Mwampaghale.
Kuuawa kwa mtu huyo kumetokea ikiwa imepita wiki moja baada ya watu wengine watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kuuawa na polisi baada ya kutokea majibizano ya risasi katika eneo la Nyabugombe kata Nyakahura wilayani Biharamulo, Desemba 01 mwaka huu saa 8 usiku.