Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Joseph Mhagama ameitaka Wizara ya Madini kuendelea kushirikiana na kamati hiyo pindi inapohitaji kufanya marekebisho katika maeneo yanayohitaji kutupiwa jicho katika Sheria ya Madini.
Ameongeza kuwa, ushirikiano huo ni muhimu kutokana na umuhimu wa Sekta ya Madini kwa maendeleo ya sekta, Taifa na mchango wake kiuchumi.
Mhagama ameyasema hayo leo Novemba 9, 2022 jijini Dodoma katika semina ya siku moja kwa kamati hiyo iliyotolewa na Wizara ya Madini ambapo wizara imepata nafasi ya kuwapitisha wajumbe wa kamati hiyo katika maeneo yanayopendekezwa kufanyiwa marekebisho katika Sheria ya Madini Sura 123 yanayolenga kuondoa mapungufu ambayo yamejitokeza katika utekelezaji wa baadhi ya masharti katika Sheria ya Madini.
‘’ Ni fursa kwetu kuzidi kuielewa sekta hii jambo ambalo litatusaidia kujua namna ya kuishauri serikali. Itatusaidia kuvifahamu vipaumbele vya wizara na kama wizara, mmefanya vema kuihusisha mapema kamati hii,’’ amesema Mhagama.
Naye, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema kutokana na sekta ya Madini kuhusisha wawekezaji kwa kiasi kikubwa, upo umuhimu wa kamati hiyo kukaa karibu na wizara
Waziri Biteko ameongeza kuwa, semina hiyo imelenga katika kubadilishana mawazo, kujenga uelewa wa pamoja katika masuala ya sheria inayosimamia sekta ya Madini ikiwemo kupokea ushauri unaotolewa na kamati hiyo kwa lengo la kuongeza tija kwenye sekta ya Madini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa akizungumza katika semina hiyo ameiomba kamati hiyo kuendelea kuitembelea wizara ili kuiwezesha kuelewa kwa kina sekta ya madini kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya taifa.
‘’ Wawekezaji wanapokuja wanapenda kuangalia mazingira ya uwekezaji, na sisi kipaumbele chetu ni madini ya kimkakati, mnapotumbelea mtatuelewa na kujua namna ya kutushauri.’’ amesema Dkt. Kiruswa.
Awali, akizungumza katika semina hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Adolf Ndunguru amesema semina hiyo inafanyika baada ya wizara kufanya marekebisho yanayopendekezwa katika Sheria ya Madini kuwezesha kusimamiwa kikamilifu kwa sekta ya madini.
Akitoa wasilisho, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Madini Julieth Moshi, ameipitisha kamati hiyo na kutoa ufafanuzi wa marekebisho yanayopendekezwa katika Sheria ya Madini Sura ya 123 kupitia Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali Na. 3 wa Mwaka 2022.