Breaking

Tuesday, 29 November 2022

WAZIRI MKUU AWASIMAMISHA KAZI WATUMISHI WAWILI KISA UBADHILIFU WA FEDHA, KUKIUKA MAADILI



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka Halmashauri nchini kuongeza umakini katika manunuzi ya vifaa vinavyotumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao ili iweze kukamilika katika muda uliopangwa na kutoa huduma kwa wananchi.

Ametoa wito huo leo (Jumanne, Novemba 29, 2022) alipozungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Wenyeviti wa Halmashauri wanapaswa kuwa wakali katika kufuatilia manunuzi ya vifaa mbalimbali na watumie wakaguzi wa ndani katika kufuatilia taarifa za manunuzi.

“Manunuzi hapa kisarawe ni ya gharama kubwa katika miradi yenu, miradi haishi kwasababu ya gharama kubwa, na bahati mbaya mnafanya hivyo kwa fedha za Serikali kuu”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kumfuatilia aliyekuwa afisa mapato katika Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe Fredy Bandai aliyehamishiwa Mtwara vijijini

“Huyu asimamishwe kazi na arejeshwe Kisarawe ili aje atolee taarifa ya fedha kiasi cha shilingi milioni 253 alizokusanya lakini hazionekani”

Pia, Waziri Mkuu amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kisarawe James Chitumbi kwa kukiuka maadili ya uongozi.

Kadhalika Waziri Mkuu amewataka wakuu wa Idara kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao “Tunataka watanzania wahudumiwe, ninyi watumishi wa umma ni wahudumu kwa wananchi wetu, fuatilieni miradi ili iweze kuleta tija kwa wananchi”

Kwa Upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt Festo Dugange amesema Rais Samia Suluhu Hassan amepekea zaidi ya shilingi bilioni 6 katika halmashauri ya wilaya ya kisarawe kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na ukarabati mkubwa wa hospitali ya wilaya.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages