Na Mathias Canal, WEST- Dodoma
Serikali inayo azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka huu wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni Mia moja kuanza ujenzi huo.
Kiasi hicho cha fedha ni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 62 kwa Wilaya ambazo zilikuwa hazijajengewa Vyuo vya Ufundi Stadi pamoja na chuo kimoja cha mkoa.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda (Mb) wakati akiongoza kikao cha Menejimenti ya Wizara pamoja na VETA kilichofanyika katika ukumbi wa VETA Jijini Dodoma leo tarehe 28 Novemba 2022.
Waziri Mkenda amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha 2022/23, Serikali imetenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 62 kwa Wilaya ambazo zilikuwa hazijajengewa Vyuo vya Ufundi Stadi.
Waziri Mkenda amesisitiza ulazima wa utekelezaji wa haraka na mkakati wa kuhakikisha ujenzi unaanza mapema na kujengwa kwa usahihi kwa kuzingatia taratibu zote husika.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema mageuzi ya elimu yanayokuja yanakwenda sambamba na kuandaa mazingira ya kuhakikisha elimu ujuzi inapatikana.
Akizungumzia ujenzi wa Kampasi za Vyuo Vikuu katika mikoa 14 kupitia Mradi wa HEET Waziri Mkenda amewataka Wakandarasi waliopo wizarani kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji na kushirikiana na Vyuo Vikuu kujua mikakati iliyowekwa na vyuo hivyo kuhusu ujenzi huo ili kazi ikamilie kwa haraka.
Kadhalika, Waziri Mkenda mesema adhma ya Serikali ni kuhakikisha kila Wilaya inakuwa na Chuo cha VETA ili vijana kuanzia shule ya msingi mpaka elimu ya juu anapomaliza masomo lazima awe na ujuzi fulani ambao utakuwa tija na kipato.
MWISHO