Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa, Maafisa Michezo na walimu wa michezo kote nchini kutekeleza agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kampeni ya mtaa kwa mtaa inayolenga kuibua vipaji vya sanaa na michezo inatekelezwa kwa ufanisi kwa kuhamasisiha michezo katika maeneo yao.
Pia amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri katika shule 56 teule za michezo kuanza kuboresha miundombinu za shule hizo wakati wakingoja fedha za umaliziaji kutoka serikalini.
Waziri Mchengerwa ametoa wito huo leo Novemba 5, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na walimu wa michezo kutoka shule teule 56 nchini Tanzania wanaoshiriki mafunzo ya michezo yaliyo andaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ikiwa ni mkakati wa Serikali wa kuboresha michezo kuanzia kwenye ngazi ya shule na kuifanya kuwa sehemu ya masomo badala ya kuchukulia kama kitu cha ziada.
Amefafanua kuwa dhamira ya Serikali ni kuona Wakurugenzi wa Halmashauri zilizopata bahati ya kuwa miongoni mwa shule hizo teule 56 kuanza kujiandaa kwa ujenzi wa miundo mbinu kama vile kuboresha viwanja na kujenga uzio katika shule hizo ili pesa ya serikali iwe ya ziada katika kuboresha miundo mbinu ya shule husika.
“Kujenga uzio kunagharimu kama milioni 70 tu, binafsi siamini kama kuna halmashauri inakosa milioni 70 kwa ajili ya kujenga uzio katika shule moja tu, kwahiyo nawaomba Wakurugenzi wa Halmashauri mtusaidie katika kuboresha miundombinu katika shule hizi 56 ambazo Mhe. Rais samia suluhu ameziridhia ziwe maalum kwa michezo.
Aidha amewataka walimu hao waliopatiwa mafunzo ya michezo kuanza mara moja kutoa mbinu za kimichezo kwa wanafunzi mara tu watakaporejea katika vituo vyao vya kazi.
"Walimu mliokuwa katika mafuzo haya mnatakiwa kujiongeza huko katika shule mnazofundisha na kutosubiri fedha za Serikali zitoke kwa ajili ya vifaa bali muanze hata kwa jogging na mazoezi mengine wakati mkisubiri fedha za Serikali" amesema Mchengerwa.
Awali akimkaribisha Waziri Mchengerwa Katibu mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Neema Msita alisema walimu hao wamepewa mafunzo ya awali kuhusiana na michezo ambayo yataendeshwa kwa muda wa siku saba, na kueleza mpango wa Baraza kuwa ni kuwapeleka katika kozi kadhaa za muda mfupi katika Chuo cha Michezo cha Malya ili kuwanoa katika masuala ya michezo.