Na Selemani Msuya
WAZALISHAJI, wafugaji na wauzaji wa vifaranga wa kuku wa nyama wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Mifugo ya Uvuvi kusitisha uingizaji wa vifaranga nchini, ili kulinda soko la ndani.
Akizungumza na Raia Mwema kwa njia ya simu, Mfugaji na Muuzaji wa Vifaranga, Amina Rashid wa Mbezi Luguruni wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam, alisema hali ya soko la kuku ni mbaya kutokana na bei kushuka, huku bei ya vifaranga na chakula ikiwa juu.
“Mimi nanunua vifaranga, nafuga na kuuza, ila changamoto kubwa kwa sasa ni soko, kwani unanunua kifaranga sh.2,000 unamgharamia kwa Sh.6,000, ukienda sokoni unauza Sh.5,500 hadi Sh.6,000, chakula cha kuku mfuko Sh.86,000 hadi Sh.90,000 na dawa zipo juu, tunaumia sana,” alisema.
Mfugaji huyo alisema taarifa alizonazo ni kwamba hali hiyo inasababishwa na uingizwaji wa vifaranga kwa njia za magendo kutoka Uganda na Malawi.
Amina alisema mwanzo alikuwa anauza boksi 50 zenye vifaranga 5,000 vya kuku, ila kwa sasa anauza boksi tano kwa mwezi, hali ambayo inamrudisha nyuma.
Kwa upande wake Muuzaji Allan Massawe alisema kilio chake kikubwa ni Serikali kushindwa kuchukua hatua kwa watu ambao wanaingiza vifaranga kwa njia ya magendo, hali ambayo inaua soko la ndani.
Massawe alisema Serikali inatangaza kusitisha utoaji wa vibali vya uingizaji vifaranga, ila kiuhalisia bado wapo watu wanaingiza.
“Unaporuhusu mtu aingize vifaranga boksi 300 ni lazima soko la ndani liathirike, hivyo tunaomba Serikali iangalie jambo hili, kwani wanaoumia ni wazalishaji wa ndani,” alisema.
Naye Mfugaji Mary Luhui wa Tabata alisema kama hatua hazitachuliwa kwa haraka, wajasirimali wadogo wataathirika na kuuawa mitaji.
“Mamlaka hazitaki kukubali kuwa watu wanaingiza vifaranga kwa njia za panya, ila madhara yake ni makubwa, soko limeyumba. Nilikuwa nafuga na kuuza kuku 3,600 kwa mwezi, ila kwa sasa hata 1,000 hawafiki na mtaji unaendelea kukata,” alisema Luhui.
Flora Kamote wa Tegeta jijini Dar es Salaam alisema yeye kama mjane anapitia wakati mgumu kutokana na biashara kuwa ngumu katika miezi ya hivi karibuni.
“Mimi ni wakala wa vifaranga kutoka Kampuni ya Organia, ila hali ya biashara ni mbaya, nauza kuku wenye wiki nane yaani miezi miwili kutoka mwezi mmoja wa awali, ni gharama kubwa kuwatunza. Nilikuwa nauza kuku 4,000 kwa mwezi lakini kwa sasa tunabahatisha,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Kuku wa Nyama Tanzania (TABROFA), Aloyce Makoye alisema biashara ya kuku wa nyama na vifaranga imeharibika kwa sasa.
“Kuna mafuriko ya kuku wanyama wanaotakiwa kuingizwa sokoni, hali ambayo imeshusha bei na matokeo yake ni mitaji ya wafugaji kutetereka. Sisi tunahisi kuna mwanya unatumika kuingiza kuku kwa njia ya panya, tunaomba mamlaka zichukue hatua, kwani tunaenda kufirisika,” alisema.
Makoye alisema hali hii haijawahi kutokea katika biashara ya kuku wa nyama kwa kampuni zote kulalamika biashara ni nguvu.
“Ukienda Interchick, Kibo, Organia, Alvin na wengine wanalalamika biashara ni ngumu, hivyo nashauri mipaka iangaliwe, kwani tunapoenda ni pabaya na vibali visitolewe,” alisema.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kuzalisha Vifaranga ya Organia, Albert Momdjian alisema wao kama wazalishaji na mawakala wanapata uchungu na hasira kwa kile kinachoendelea katika sekta ya kuku nchini Tanzania.
Alisema jitihada za baadhi ya watu kuharibu ukuaji wa sekta hiyo zimebainishwa na kwamba hawatakaa na kukubali majaribio hayo ya kuharibu jamii ya wafugaji wa kuku wa Kitanzania kwa njia hiyo.
“Tunawasikia na kuhisi maumivu na hasira zenu. Tutaendelea kuwasaidia wakulima na mawakala wetu wote, hasa katika nyakati hizi ngumu. Tutahakikisha sauti zenu zinasikika na katika ngazi za juu zaidi nchini. Tunashirikiana na idadi kubwa ya wadau. Vuta subira yajayo ni mazuri. Organia Ltd ni fahari ya Tanzania,” alisema.
Akizungumzia malalamiko hayo Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo ambaye ndiye mtoaji wa vibali vya kuingiza mifugo ikiwemo vifaranga, Profesa Hezron Nonga, alikanusha taarifa za wizara kutoa vibali vipya vya uingizaji wa vifaranga nchini.
Prof. Nonga alisema hadi sasa kampuni zinazoingiza vifaranga ni mbili ambazo ni Wolowolo Animal Care Center na The One Agro Enterprise ambazo zilipata vibali kuanzia mwaka jana na kwamba vifaranga vinavyoingizwa ni katika kumalizia maombi yao za zamani.
“Hizi kampuni ziliomba vibali katika kipindi ambacho nchi ilikuwa na changamoto ya uhaba wa vifaranga ambapo The One Agro Enterprise imeruhusiwa kuingiza vifanga 494,000 kutoka Uganda na Wolowolo vifafanga 150,000 kutoka Malawi na mwisho wakuingiza ni Januari 15,2023,” alisema.
Aidha, alisema kushuka kwa bei ya kuku katika soko kunatokana na kipindi husika na hali ya uchumi na kwamba matarajio yao ni kuanzia mwezi Disemba biashara itakuwa nzuri zaidi.
Mkurugenzi huyo alisema Serikali ipo macho kufuatilia watu wanaoingiza vifaranga kwa njia za panya, ili kulinda wazalishaji wa ndani.
Alitoa ushauri kwa kampuni za uzalishaji wa vifaranga kuzingatia ubora wa vifaranga ili kuwa na ushindani katika soko.
Mwisho