Breaking

Tuesday, 29 November 2022

WATENDAJI, WADAU WA MICHEZO WATAKIWA KUBADILIKA KUIWEZESHA TANZANIA KUSHIRIKI KOMBE LA DUNIA



Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka watendaji na wadau wa michezo nchini kubadili fikra, mtazamo na utendaji wao ili Tanzania iweze kushiriki Kombe la Dunia ifikapo 2030.

Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Novemba 28, 2022 uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam wakati akiwaaga na kuwakabidhi bendera ya Taifa washindi wa Tigo wanaokwenda kwenye mashindano ya Soka ya Kombe la Dunia nchini Qatar.

" Inawezekana kama kila mmoja wetu kwenye sekta ya michezo akibadilika na akiweka mbele uzalendo na utaifa tutasonga mbele na kushinda Kombe la Dunia 2030 Kwa kuwa Rais wetu amekuwa akituhamasisha kufanya uwekezaji mkubwa kwenye michezo" amefafanua Mhe Mchengerwa


Aidha, amesema endapo watendaji wa Serikali kwenye sekta ya michezo hawatabadilika atakwenda kuchukua maamuzi magumu.

Amewataka washindi hao waliopata bahati ya kwenda kwenye Kombe la Dunia kuitangaza Tanzania.


Ameongeza kuwa katika kipindi hiki tayari Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya michezo nchini ikiwa na viwanja vikubwa saba katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha na Mbeya.

Waziri Mchengerwa amehoji kama Timu ya Wanawake ya Soka chini ya umri wa miaka 17 Serengeti girls iliweza kufuzu kuingia robo fainali Kombe la Dunia hakuna sababu ya timu ya taifa kutofanya vizuri.


Amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwafadhili watu kwenda Kombe la Dunia kama inavyofanya kampuni ya Tigo.

Kampuni ya simu ya mkononi Tigo imetoa ufadhili kwa watu 50 kwenda Qatar kuangalia Kombe la Dunia ambapo katika awamu ya kwanza watu kumi wameondoka leo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages