Breaking

Friday, 11 November 2022

WADAU MBEGU ASILI WATAKIWA KUJIKITA KWENYE TAFITI



Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MWENYEKITI wa Shirika la Kuendeleza Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Dk Mwatima Juma amewataka wadau wa mbegu asili na zilizosahulika kujikita kwenye utafiti, ili kuweza kushawishi mamlaka kwanini wanataka mbegu hizo kupewa kipaumbele.

Dk Mwatima ametoa rai hiyo jana wakati akizungumza na wadau hao waliokutana kwa siku tatu jijini Dodoma katika kongamano la kujadili hatma ya mbegu asili na zilizosahaulika hapa nchini na duniani kwa ujumla.

Mkutano huu umeshirikisha wadau kutoka Shirika la SWISSAID Tanzania, Alliance for Food Sovereignty in Afrika (AFSA), TOAM, Shirika la Kuendeleza Kilimo Hai Barani Afrika (AFRONET), PELUM Tanzania, Mkulima Mbunifu, Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania (SAT), ECHO East Afrika na wengine.





Mwenyekiti huyo alisema kuzungumza na kuhamasisha kilimo hai cha kutumia mbegu asili kila siku, kunaweza kuwa na matokeo chanya iwapo kutakuwa na taarifa za kitafiti.

“Hawa wafanya maamuzi wana mambo mengi, jambo la kusisitiza na kuwabana ni sisi wadau wa mbegu asili kuonesha ushahidi wa kitafiti za kisayansi ambazo zitaweza kuwashawishi kuweka mkazo katika eneo hilo,” alisema.

Dk. Mwatima alisema kila taasisi ambayo inahamasisha matumizi ya mbegu asili inapaswa kutenga fedha kwa ajili ya utafiti, pamoja na kutoa elimu kwa wakulima umuhimu wa mbegu hizo.

Alisema pamoja na utafiti ambao unatakiwa kufanyika ni vema kuonesha athari ambazo ardhi imepata kupitia kilimo ambacho hakitegemei mbegu asili.

Mwenyekiti huyo alisema iwapo kundi hilo la mbegu asili litakuwa na misimamo ya pamoja katika kupigania kilimo hai cha kutumia mbegu asili ni wazi kuwa ajenda hiyo itaweza kunusuru jamii na taifa kwa ujumla.







Katika hatua nyingine, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kuendeleza Kilimohai Barani Afrika (AfrONet) Constantine Akitanda, amekieleza kikao cha wadau wa mbegu mjini hapa kuwa bara la Afrika lina kila sababu ya kuzalisha chakula cha kutosheleza mahitaji ya watu wake wote.

“Ni lazima nchi ijielekeze katika kuongeza uzalishaji wa mazao yaliyotelekezwa ama mazao yatima, mazao haya yana nutrisheni ya kutosha na ni miongoni mwa mazao yanayohimili ukame, yanastawi hata katika ardhi isiyo na rutuba ya kutosha na kuhimili magonjwa” alisema.


Akitanda alisema kufuatia mabadiliko ya tabianchi kuendelea kuiathiri dunia, uzalishaji wa mazao yaliyozoeleka kama mahindi, mpunga na ngano ambao kwa sehemu kubwa unategemea mvua, ni wazi kwamba mahitaji ya kujitathimini ni makubwa zaidi ili kuwa na mkatati thabiti wa kupanua wigo wa mazao yatima.



Tanzania kama zilivyo nchi nyingine za Kiafrika lazima iwe mstari wa mbele ili isiachwe nyuma katika kujihakikishia usalama wa chakula siku za mbeleni.

Mwisho
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages