Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe.Mohamed Mchengerwa amezindua Tamasha la Msimu wa Utamaduni wa Afrika Kusini na Tanzania litakalofanyika nchini kwa wiki moja katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma na Zanzibar,linalokwenda kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali.
Mhe. Mchengerwa amezindua Tamasha hilo usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam ambapo amesema ushirikiano wa Tanzania na Afrika Kusini umedumu kwa muda mrefu ambapo Wazee wetu Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Nelson Mandela wa Afrika Kusini waliuasisi ushirikiano huo toka enzi za kupigania uhuru wanchi hizi.
"Aidha, wakati wa harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika, Tanzania chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere ilikuwa ngome na kitovu cha harakati za kupigania uhuru. Vyama vya ukombozi kutoka nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo ANC na PAC vya Afrika Kusini vilipata mafunzo ya kupigania uhuru nchini Tanzania kutoka mwaka 1964-1994." Amefafanua Mhe, Mchengerwa
Ameongeza kuwa, tangu wakati huo, Tanzania na Afrika Kusini wameendelea kuwa nchi rafiki katika Sekta mbalimbali ikiwemo Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Waziri Mchengerwa ameeleza kuwa Tamasha la msimu wa utamaduni linajumuisha shughuli mbalimbali za Sanaa na Utamaduni ikiwemo, Maonesho ya harakati za Ukombozi, Sanaa za ufundi za Afrika Kusini na Tanzania, ngoma za asili, maonesho ya Filamu za Tanzania na Afrika Kusini, uchoraji wa kiubunifu na kutembelea maeneo yenye historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Dodoma.
Amesema, hiyo itawapa wageni na watanzania fursa ya kujifunza historia ya mapambano ya kudai uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika na kujionea urithi mkubwa wa historia uliosalia katika nchi yetu.
Aidha, amesisitiza kwamba Tamasha la Msimu wa Utamaduni ni jukwaa muhimu la kuonesha na kutangaza bidhaa za kiutamaduni za kiafrika kupitia maonesho ya kazi za mikono za utamaduni na ubunifu, matembezi ya kiutamaduni, muziki wa kiafrika pamoja na ngoma za asili.
"Tanzania ndio nchi pekee yenye historia ya uhifadhi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, vijana wanapaswa kutambua kuwa Taifa letu lilitoa machozi, jasho na damu kuhakikisha Afrika Kusini na Mataifa mengine ya Afrika yanakua huru" alisema Mhe. Mchengerwa.
Ameongeza kuwa, Tamasha hilo litaimarisha undugu wa nchi hizo na kukuza Sekta za Utamaduni na Sanaa ikiwa ni pamoja na kutangaza Utalii, Mila na Desturi za nchi hizo, ambapo amesisitiza wadau wa sekta hizo kujitokeza kuuza na kuonesha bidhaa zao katika msimu wa Tamasha hilo.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Samia imeendelea kuboresha Sekta hizo ambazo zimeajiri vijana wengi, huku akitoa wito kwa Sekta Binafsi kuunga mkono juhudi hizo.
Aidha, Mhe. Mchengerwa ametoa wito wa Idara ya Utamaduni kuhakikisha inaandaa matamasha yenye sura ya kimataifa ambayo yatahusisha nchi nyingi zaidi.
Awali Naibu Waziri wa Utamaduni wa Afrika Kusini Mhe. Mcawe Mafu alisema nchi yake imeleta Tamasha hilo limeletewa Tanzania kwakua nchi hizo ni ndugu wa muda mrefu.