Meneja ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Ziwa, Musa Kuzumila amesema kuwa maji na tope la bwawa la Mgodi wa Almasi wa Williamson Diamond Ltd (WDL) havina madhara yoyote hivyo wananchi wanaruhusiwa kutumia na kunywesha mifugo kama kawaida.
Maji na tope hilo yametokana na bwawa la majitaka la mgodi huo unaomilikiwa na kampuni hiyo (asilimia 75) na Serikali (asilimia 25) kupasuka Novemba 7 mwaka huu na kutiririsha maji hayo yenye tope kwenye makazi ya watu.
Related : DKT. BITEKO AUAGIZA MGODI WA ALMASI MWADUI KUKAMILISHA TATHMINI KUBOMOKA BWAWA LA TOPE
Akitoa taarifa ya uchunguzi leo Jumamosi Novemba 12, 2022 katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Kuzumila amesema baada ya kufanya upimaji walibaini kuwa maji na tope hilo havina madhara ya aina yeyote.
"Tulianza upimaji wa sampuli Novemba 9 baada ya tukio hili kutokea tulipima maji na tope ambapo tulichukua maji magharibi mwa bwawa la almas na upande wa kwenye vijiji vilivyoathirika, hivyo tulibaini tope na maji hayana kemikali ya aina yoyote, maji hayo yapo salama hivyo tunawaomba wananchi wasiwe na hofu tena,"amesema Kuzumila.
Kwa upande wake meneja wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Ziwa Mwanza, Jarome Kayombo amesema kuna uchunguzi mbalimbali umefanyika kuhusiana na bwawa hilo kupasuka ofisi ya mkemia wamepima wameona maji hayo hayana madhara kwa wananchi na kwa wanyama.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema amesema baada ya bwawa kupasuka maji yakatiririka wananchi walishindwa kutumia maji kwa kuhofia yana madhara, lakini vipimo vimeonyesha maji haya ni salama, hivyo wanatakiwa kutumia bila wasiwasi.
Soma zaidi >>HAPA<<
Via: Shinyanga Press Club