Serikali itaendelea kuimarisha doria za kudhibiti wanyamapori waharibifu wakiwemo tumbili na nyani wanaokula mazao na kuharibu mashamba ya wananchi.
Hayo yamesemwa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Sengerema, Mhe. Tabasam Mwangao aliyetaka kujua lini Serikali itawavuna tumbili katika Kisiwa cha Juma wilayani Sengerema.
Amesema Serikali imefanya kazi ya kuyabaini na kuyadhibiti makundi ya tumbili yanayosumbua wananchi katika Kisiwa cha Juma Wilayani Sengerema.
Aidha, Naibu Waziri Masanja amesema Serikali itaendelea kuhamisha makundi hayo ya tumbili na kuyapeleka katika hifadhi nyingine zenye mahitaji ya wanyamapori .
Ameongeza kuwa Serikali imetoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mbinu rafiki za kufukuza tumbili katika mashamba.
Akijibu swali la Mbunge wa Igalula, Mhe. Daud Venant kuhusu mpango wa Serikali wa kuongeza maeneo kutoka hifadhi ya Msitu wa Uyui Kigwa Rubuga katika Jimbo la Igalula, Mhe. Masanja ameelekeza vijiji vya eneo hilo kuandaa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi ili kuepuka migogoro ya ardhi.
Pia, amefafanua kuwa Serikali haioni haja ya kumega eneo kutoka kwenye hifadhi hiyo kwa ajili ya kuwagawia wananchi kutokana na umuhimu wa hifadhi hiyo kiikolojia.