Breaking

Thursday, 10 November 2022

“SERIKALI INAENDELEA KUWEKA MAZINGIRA MAZURI YA UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI” – DKT. KIRUSWA





Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini inaendelea kuweka mazingira mazuri kupitia sheria na kanuni za madini ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika na Sekta ya madini.

Dkt. Kiruswa ameyasema hayo leo tarehe 10 Novemba, 2022 jijini Dodoma kwenye semina ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyoandaliwa na Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini yenye lengo la kuwapa uelewa wa majukumu yanayofanywa na kampuni inayotoa huduma za manunuzi na ugavi kwenye migodi ya madini ya TCL Services Limited.

Semina hiyo imeshirikisha pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adolf Ndunguru, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Madini, Augustine Ollal, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Madini, Issa Nchasi, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula na watendaji wengine kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.

Amesema kuwa ili kuhakikisha watanzania wote wananufaika na uwekezaji wa kampuni za madini kwenye Sekta ya Madini, Wizara kupita Tume ya Madini imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi wanaoishi karibu na migodi ya madini.

Awali akizungumza katika semina hiyo, Mtendaji Mkuu wa kampuni ya TCL Services Limited, Martin Swanepoel amesema kuwa kampuni yake inayotoa huduma za manunuzi katika migodi ya madini ya North Mara na Bulyanhulu tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikitoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa bidhaa za watoa huduma kutoka katika bandari ya Dar es Salaam hadi kwenye migodi ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha watoa huduma na wamiliki wa migodi huku ikihakikisha kila upande unanufaika.

“Lengo letu kuu ni kutoa huduma ya kuunganisha kampuni za madini na watoa huduma kwa kuhakikisha kampuni na watoa huduma wananufaika kwa pamoja,” amesema Swanepoel

Katika hatua nyingine, wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeitaka kampuni ya TCL Services Limited kuimarisha mahusiano yake na jamii inayozunguka migodi ya madini inayohudumia.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages