Breaking

Friday, 11 November 2022

"SANAA INAONGOZA UKUAJI UCHUMI NCHINI" - DKT. MPANGO



Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali imefanya maboresho makubwa kwenye Tamasha la mwaka huu la 41 la Utamaduni na Sanaa Bagamoyo kuwa la kimataifa ambapo limeshirikisha nchi mbalimbali duniani ili kuitangaza Tanzania na utamaduni wake duniani.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akimkaribisha Makamu wa Rais Mhe, Dkt. Philipo Mpango kuzindua rasmi tamasha hili kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano. Mhe. Samia Suluhu Hassan.


Ameongeza kuwa tamasha hili limeshirikisha vikundi vya wasanii kutoa mataifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Canada, Zambia, Burundi na Visiwa vya Mayote kutoka nchini Ufaransa.

“Mwaka huu tumeendelea kuliboresha Zaidi tamasha hili kutoka kuwa tamasha la mazoea la wanafunzi wa sanaa hapa chuoni ili kulipatia hadhi zaidi ya kuwa tamasha la kimataifa.” Amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Aidha amesema wameteleza maelekezo ya Mhe. Rais ya kutaka kuendeleza tamasha hili na lile la Sauti za Busara kutoka Zanzibar ili kuyafanya ya kimataifa, ili yasaidie kulitangaza taifa duniani.



Aidha, Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa Wizara imeanza kutelekeza program ya mtaa kwa mtaa nchi nzima ya kusaka vijana wenye vipaji katika sekta ya Sanaa na Michezo kwa lengo la kuvikuza na kuviendeleza.

Akitoa hotuba yake, Mhe. Mpango ameipongeza Wizara kwa kazi kubwa inayofanya ambapo amesema kwa sasa tasnia ya burudani imeongoza kwa kukua kwenye uchumi kwa asilimia 19 katika mwaka uliopita.



Ametoa rai kwa wasanii wa muziki na filamu kuzingatia maadili na miongozo ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Bodi ya Filamu Tanzania kwa kutengeneza maudhui ya kazi huku wakikumbuka kuwa wasanii ni kioo cha jamii na kwamba wakitengeneza kazi mbaya jamii haitaheshimu kazi zao.

Akizungumzia kuhusu agizo la Mhe. Rais alilolitoa Ikulu kwa timu ya taifa ya Serengeti Girls Julai 2022 kuhusu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara ya Fedha na Mipango kujadiliana juu ya namna bora ya kuongeza bajeti ya Wizara ya Utamaduni ili shughuli muhimu zitakazochagiza ukuaji wa uchumi na ajira kwa vijana kupitia sekta hizi za burudani zisikwame, ameagiza apate utekelezaji huo ifikapo Desemba 30 mwaka huu.Mbali na hiyo Mhe. Mpango ametoa maelekezo kadhaa kwa wizara ya kusaidia kuboresha sekta ili iweze kutoa mchango kwa taifa.

Tamasha hili lilianza jana kwa kufanya kongamano la sanaa na uchumi ambapo wadau mbalimbali wa sekta walijadili kwa kina, na kufuatia na usiku wa burudani kali kutoka mataifa mbalimbali ambapo leo pia kutakuwa na burudani nyingi wakati kesho tamasha litatamatisha kwa kuwa na Bagamoyo Royal Tour na burudani.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages