Wakazi wa mtaa wa Shibayi kata ya Buhongwa wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza wamepata taharuki baada ya kuona mwili wa kichanga kinachokadiriwa kuwa na umri wa miezi sita ukiwa umewekwa kwenye boksi na kutupwa katika dampo lilipo kwenye soko la mtaa huo.
Mwili huo unadaiwa kutupwa leo majira ya asubuhi kwenye dampo ambapo watu waliokuwa wanaokota mabaki ya chakula waliupata mwili huo kwenye boksi moja ndani ya dampo hilo.
‘Sasa ile kukimbilia lile toroli tukaanza kuchambua chambua sasa kuna mwezetu akakimbilia boksi akaanza kuchambua nikamuuliza sasa hilo boksi umepata na manguo akasema ehh akaendelea kulichambua baadae akanyamaza mimi nikamuambia umeangalia kuna nini? Akasema kuna mtoto nikamuuliza kweli? Nikaenda kuangalia nikakuta kweli kuna mtoto ndio tukaanza kuwaambia watu’ amesema moja ya shuhuda Joyce Muna
Akizungumza kwa njia ya simu afisa mtendaji wa kata ya Buhongwa Heaven Mauki amesema tukio hilo ni kwanza kutokea katika kata hiyo na kwamba kwa sasa mwili wa kichanga hicho umechukuliwa na jeshi la polisi na umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mwanza Sekou toure.
Via: EATV