Wakazi wa Wilaya ya Temeke na Kinondoni na maeneo ya katikati ya Jiji wameanza kunufaika na huduma ya majisafi kutoka katika mradi wa maji Kigamboni uliozinduliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassani.
Mradi wa maji Kigamboni umesaidia kupunguza adha ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo hayo katika kipindi cha kiangazi ambapo kupitia mradi huu wananchi sasa wanapata huduma.
Akizungumzia hali ya upatikanaji maji katika wilaya ya Temeke, Meneja wa DAWASA Temeke, ndugu Crossman Makere ameeleza kuwa hali ya huduma kwa sasa inaridhisha katika maeneo mengi huku huduma ikiendelea kuimarika huku akiwataka wananchi kuendelea kuwa watulivu kwani Mamlaka imejipanga kuhudumia wananchi wote bila upendeleo.
"Tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huduma ya maji kutoka mradi wa Kigamboni imekuwa suluhisho kwa kiasi kikubwa katika Wilaya yetu ya Temeke, maeneo yaliyokuwa yakikosa huduma awali kutokana na ukame wa muda mrefu sasa yanapata huduma na shughuli za uzalishaji na maendeleo zinatekelezwa kwa kasi."ameeleza ndugu Makere.
Makere ametoa rai kwa Wananchi kuendelea kuwa wavumilivu kwani watendaji wa DAWASA wapo kazini usiku na mchana kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya majisafi.
Naye, Ndugu Nora Magege mkazi wa Uhamiaji-Kurasini ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kutatua changamoto ya maji Kwa wakati na sasa wanapata maji ya uhakika.
"Hapo awali baada ya upungufu wa maji uliotokana na ukame kuanza tulipata changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji, hata wakati wa mgao tulikuwa tunapata sana changamoto. Tunasgukuru sasa huduma imeimarika na sasa tunafurahia tena huduma hii" ameeleza ndugu Magege
Kwa upande wake Halima Mkwame mkazi wa Tandale kwa Mtogole amesema kupatikana kwa huduma ya maji katika mtaa wao kumeleta furaha kubwa hasa kwa wanawake ambao muda mwingi iliwalazimu kwenda mbali kutafuta huduma hiyo.