Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mchimbaji na mnunuzi wa madini, Ezekia Luhwesha (31) kwa tuhuma za mauaji ya wakala wa maegesho ya magari aitwaye William Mgaya (58).
Akithibitisha tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema mtuhumiwa huyo ambaye ni mkazi wa Matundasi Wilayani Chunya anatuhumiwa kumuua Mgaya kwa kumpiga risasi.
Kamanda Kuzaga amesema kuwa mnamo Novemba 26, 2022 majira ya saa 04:30 asubuhi huko maeneo ya Mafiati ofisi ya TARURA iliyopo Kata ya Ruanda, Jijini Mbeya, William Mgaya akiwa na mwenzake Almas Shaban (32) wakiwa katika kazi yao ya kukusanya ushuru walimkamata mtuhumiwa Ezekia Luhwesha baada ya ku scan namba yake ya Gari T.772 DVY Toyota Hilux na kugundua kuwa Gari hilo lina deni la Tshs.7,500/=.
Mtuhumiwa alitakiwa kulipa deni hilo lakini alihitaji kuona hilo deni linatokana na maegesho gani hivyo kulazimika kuongozana naye hadi zilipo ofisi za TARURA kwa ajili kuangalia kwenye mfumo ili kupata taarifa za deni hilo.
"Mtuhumiwa alionyeshwa taarifa za deni hilo na kuridhika kuahidi kulipa deni hilo lakini wakala Mgaya alimtaka kulipa deni hilo papo hapo kutokana na deni hilo kuwa la muda mrefu" Ameeleza Kamanda Kuzaga
Kamanda Kuzaga amesema kuwa yalitokea majibizano kati ya marehemu na mtuhumiwa hali iliyopelekea mtuhumiwa kutoa silaha yake Pistol na kufyetua risasi moja uelekeo alipokuwa Mgaya na kumpiga sehemu ya kifuani upande wa kulia hali iloyopeleka kusababisha kifo chake muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa Mbeya.
"Mtuhumiwa pamoja na Silaha Pistol aina ya Tisasi yenye namba T.0620-19J0037 ya mtuhumiwa ikiwa na risasi 09 ndani ya magazine anashikiliwa na Jeshi la Polisi." Amefafanua Kamanda Kuzaga
Aidha Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa wanaomiliki silaha kuzingatia masharti ya umilikishwaji wa silaha hizo.