Breaking

Saturday, 5 November 2022

MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA YANACHANGIA VIFO Mil. 41



Na. WAF - Mwanza

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2016 zinaonesha kuwa Magonjwa Yasiyoambukiza yanachangia zaidi vifo Mil. 41 ambayo ni sawa na asilimia 71 ya vifo vyote ambapo Tanzania inafikia asilimia 40.

Takwimu hizo amezibainisha Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Bw. Hassan Masala leo wakati akizindua rasmi wiki ya Magonjwa Yasiyoambikiza akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima kwenye viwanja vya CCM Kirumba Jijini Mwanza.

Bw. Masala amesema ili kuepukana na magonjwa Yasiyoambukiza inatupasa kufanya mambo kadhaa ikiwemo kufanya mazoezi ya mwili na kuepuka msongo wa mawazo.

"Pia kupunguza au kuacha matumizi ya pombe, tumbaku na dawa za kulevya pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya kutumia barabara na vyombo vya moto ili kuepuka ajali za barabarani." Amesema Bw. Masala.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya Bw. Masala amewakumbusha Watanzania juu ya tishio la Ebola na UVIKO-19 kwa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa hayo ikiwemo kunawa mikono kwa usahihi.

"Kwa sasa inaonekana bado watu wengi hususani wenye umri mkubwa na wenye magonjwa yasiyoambukiza ndio wanaathirika zaidi hivyo tuendelee kuchukua tahadhari ili tujikinge na tuwakinge wapendwa wetu." Amesema Bw. Masala.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza Dkt. James kiologwe akiwakilisha Wizara ya Afya katika uzinduzi huo wa wiki ya magonjwa yasiyoambukiza amebainisha kuwa Takwimu zinaonesha watu Mil. 500 Dunia wapo katika hatari ya kupata Magonjwa hayo kwasababu ya kuwa na Tabia Bwete.

"Kutokana na ongezeko kubwa la magonjwa yasioyoambukiza tunashauri sana watu wawe na tabia ya kufanya mazoezi ili kiuimarisha Afya za miili yetu." Amesema Dkt. Kiologwe

Pia, Dkt. Kiologwe amesema nchini kwetu inakadiriwa kuwa watu Mil. 15 na Laki Sita wapo katika hatari ya kupata Magonjwa na watu Mil. Tano na Laki Sita wapo katika hatari kubwa zaidi sababu ya kupata magonjwa hayo kama Saratani, Moyo, Kisukari na Mfumo wa Upumiaji.

Ili kuongeza kasi ya udhibiti wa Magonjwa Yasioambukiza, maadhimisho hayo hufanyika kila wiki ya Pili ya Mwezi Novemba kuwa Wiki maalumu ya Kitaifa ya kudhibiti Magonjwa hayo kwa kutoa elimu ya Afya inayohusu magonjwa mbalimbali ambayo yamekuwa tishio kwenye jamii ya Tanzania.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages