Musa Hassaji mwenye umri wa miaka 67, anaweza kuelezewa kama baba wa mataifa mengi kutokana na idadi ya watoto aliowazaa.
Musa mwenye umri wa miaka 67, anajivunia kuwa baba wa watoto 98 aliowazaa na wake 10 aliowaoa, na jumla ya wajukuu 568.
Hii ina maana kwamba kila mke wake alimzaliwa watoto wasiopungua tisa kama alivyohojiwa na Afrimax English.
Familia ya Musa ndiyo kubwa zaidi nchini Uganda, ambayo ilianza alipomzaa mtoto wake wa kwanza akiwa na umri wa miaka 17.
Mwanaume huyo mwenye wake wengi anaishi nyumba moja na wake zake wote lakini amejenga nyumba nyingine ndogo kwa ajili ya watoto wake karibu na boma kubwa analomiliki.
“Hawa watu wote unaowaona hapa ni familia yangu. Nilizaa watoto 98 na wanawake 10,” alisema kwa majivuno.
Baadhi ya watoto wake ni watu wazima na pia wameolewa, huku wadogo wangali shuleni.
Huenda kinaya katika hadithi ya Musa ni kuwa alizaliwa katika familia ya watoto wawili tu lakini walitatizika kupata riziki.
Licha ya kulelewa katika maisha ya umaskini na kuacha shule akiwa darasa la sita, Musa alifanikiwa kujiingiza katika biashara na kupata utajiri wake.
“Nilitajirika sana hivi kwamba kila familia ambayo nilibisha hodi na kuomba mchumba walinipa mara moja,” alisema.
Musa alifichua kuwa mke wake mdogo Kakazi ni mdogo kuliko baadhi ya wajukuu zake, akiongeza kuwa anaweza kuwatofautisha watoto wake lakini hajui majina yao yote.
Wake za Musa wanaonekana kuwa na mawazo sawa na mwanahabari wa Kenya Stephen Letoo ambaye hivi majuzi aliwashauri wanawake kuwakubalia waume zao kuwa na wake wengi.
Mwanahabari huyo alibainisha kuwa ni kawaida kwa wanaume kuwa na wake wengi na wanawake wanapaswa kuwafahamu wake wenza wao.