Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA Maalum la Serikali ya Jamhuri ya Korea (KOICA) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), yanatarajia kutoa dola za Marekani milioni 6.42 kwa ajili ya kuwanufaisha wakulima 20,000 wa Program ya Kilimo Tija Kigoma (KITIKI) na wakimbizi 208,000 katika kambi za Nduta na Nyarugusu mkoani Kigoma.
Taarifa ya mashirika hayo imetolewa na Mkurugenzi Mkazi wa KOICA Tanzania, Kyucheol Eo na Mkurugenzi Mkazi WFP Sarah Gordon Gibson wakati wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo ya miaka minne, Mwakilishi Mkazi wa KOICA, Eo alisema shirika hilo linatarajia kutoa dola za Marekani milioni 6 kwa ajili ya wakulima 20,000 wa Wiyala ya Kokonko, Kasulu na Kibondo mkoani Kigoma
Eo amesema fedha hizo zitawezesha kilimo kuwa bora na takribani wakimbizi 208,000 katika Kambi za Nduta na Nyarugusu watanufaika na mradi huu, kuanzia mwaka huu hadi mwaka 2027.
“Mradi huu utawawezesha wakulima wadogo kuzalisha tani za ujazo takribani 1,380 kunde, na kuwauzia wakimbizi. Pia utasaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno kwa wakulima wadogo na kuimarisha uhusiano mzuri kati ya wakimbizi na jamii inayowazunguka,” amesema..
Mkurugenzi huyo amesema hashaka kuwa mradi huu utakidhi mahitaji ya wananchi wa Tanzania ya ustawi kwa upande mmoja na amani kwa wakimbizi na jamii inayowazunguka wakimbizi.
Amesema umaskini ni changamoto kubwa katika Mkoa wa Kigoma, hivyo matarajio yake ni kuona mradi huo unachangia katika kupunguza umaskini na kuongeza kipato kwa wakulima na kuimarisha uhusiano mwema wa wakimbizi na jamii.
“Kadri ambavyo nimekuwa nikifanya kazi nchini Tanzania, ndivyo ambavyo nimekuwa nikibaini kuwa ndoto za wakulima na watoto wao hapa Tanzania, haziko tofauti na ndoto zangu nilipokuwa mtoto, kijana na hata nilivyo sasa,” amesema.
Aidha, amesema mradi huo unalenga kuisaidia Serikali ya Tanzania kutokomeza njaa, kufikia usawa wa jinsia na kuendeleza amani na usalama katika wilaya zinazohifadhi wakimbizi.
Eo amesema Serikali ya Korea, kupitia KOICA, inakusudia kufikia lengo hilo kwa kuimarisha uhakika wa chakula na lishe miongoni mwa watu walio hatarini, kama vile wakimbizi na jamii inayowazunguka.
Naye Mwakilishi Mkazi wa WFP, Gordon amesema tukio la jana limeanzisha safari ya ushirikiano wa miaka minne wa kusaidia watu walio katika mazingira magumu nchini Tanzania na wakimbizi kutoka Burundi na Kongo ambapo watatoa dola 420,000.
“Ninaamini mradi huu ni mfano bora wa jinsi misaada ya kibinadamu na maendeleo inavyosaidia na kuchangia mshikamano wa kijamii kati ya jamii mbili zinazoishi bega kwa bega. WFP na Korea tuna uhusiano mzuri ambao ulianza miaka ya 1960.
Kwa uzoefu wao wa kipekee wa maendeleo ya haraka ya kiuchumi na kijamii, Korea imeonesha kuwa kufikia njaa sifuri, ambalo ni jukumu la msingi la WFP inawezekana. Nchi hii ya Korea imehitimu kutoka orodha ya nchi zilizokua zikipokea misaada kutoka WFP na kuwa moja ya nchi wafadhili wakubwa wa WFP,” amesema.
Amesema mwezi Julai mwaka huu, WFP ilianza kutekeleza Mpango Mkakati wake wa miaka mitano ambao utasaidia kuchangia maendeleo katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kimazingira ya usalama wa chakula na lishe kwa watu wanaowahudumia, kupitia shughuli mbalimbali.
Gordon amesema mpango huo utasaidia kuendeleza ukuaji wa uchumi jumuishi kupitia hatua za soko, kuimarisha mtaji wa binadamu na kuongezeka kwa uwezo wa lishe bora, na kuhamasisha na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uboreshaji wa mazingira.
Mwisho