KIWANDA cha wachina kilichopo Nhelegani Kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga cha Jielong cha uzalishaji mafuta ya kupikia kwa kutumia malighafi ya Mbegu za zao la Pamba kimeungua moto.
Tukio hilo limetokea jana majira ya saa 10 jioni, wakati wafanyakazi wa kiwanda hicho wakiendelea na shughuli ndipo kukatokea moto huo, huku wafanya kazi wanne wakijeruhiwa na kukimbizwa Hospitali.
Mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda hicho Thomas Mayunga, amesema wakati wakiendelea na majukumu yao, na ilipofika majira hayo ya saa 10 jioni mashine moja ilipata changamoto kuingiliwa na mchanga, ndipo kukatokea msuguano na kisha moto kuanza kuwaka.
Naye msemaji wa kiwanda hicho Qi, Fengzhou rai wa china, amesema hakuna madhara makubwa ambayo yametokea kwenye kiwanda hicho, huku akishukuru Jeshi la Zima Moto na uokoaji kwa kufika kwa wakati na kufanikiwa kuuzima moto huo.
Kwa upande wake Mrakibu wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoani Shinyanga Ramadhani Kano, amesema walivyopata taarifa za tukio la moto walifika mapema, huku wakiomba msaada pia wa magari ya kuzimia moto kutoka makapuni binafsi ya Gaki na Jambo na kufanikiwa kuuzima moto huo.
Amesema hakuna madhara makubwa ambayo yametokea isipokuwa wafanya kazi wanne ndiyo wamepata majeraha na wapo hospitalini kwa matibabu, huku chanzo cha moto huo bado wanaendelea kukichunguza.
Via : Shinyanga Press Club Blog