Breaking

Friday, 25 November 2022

JAMBAZI SUGU AKAMATWA DAR




Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemkamata Jambazi Sugu Johson Omary Mchomme (39) Dereva bodaboda wakati mwingine anafahamika kama Athumani Rashid Amir maarufu kama akon akituhumiwa yeye na wenzake kujihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwa ni pamoja na kutenda makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.

Akithibitisha hilo mbele ya waandishi wa habari Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam ACP Jumanne Muliro amesema kuwa mnamo Novemba 24, 2022 saa 12 jioni katikati ya Kisarawe na Kwembe, Wilaya ya Ubungo mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa anajiandaa kwenda kuungana na wenzake ili wafanye uhalifu.


"alipobaini kuzingirwa na askari Polisi alitoa bastola yake iliyokuwa kwenye begi dogo jekundu na kupiga risasi kuwashambulia askari, na katika mazingira hayo askari walijihami na kumpiga risasi moja iliyomjeruhi mguuni na kufanikiwa kumkamata" Ameeleza Kamanda Muliro

Kamanda Muliro amesema mahojiano ya awali na mtuhumiwa huyo yalianza huku akiwa anapelekwa hospitali, alieleza kushiriki katika matukio ya uhalifu maeneo ya Jeti - lumo, Kibamba, Chanika na maeneo mengine, mbalimbali ya Jiji na mikoa ya jirani, akiwa na wenzake.

"Alieleza pia waliwahi kuvamia nyumba moja maeneo ya Chanika na kumjeruhi, mwenye nyumba kwa panga na kufanikiwa kupora pesa na bastola hiyo aina ya Fatih- 13 yenye Maker’s NO. T0620 – 10J004070 na TZ CAR N0. 95973" amefafanua Kamanda Muliro

Aidha katika upekuzi mtuhumiwa huyo amekutwa na hati ya kusafiria ya Tanzania na kadi ya mpiga kura yenye majina ya Johson Omary Mchomme zikiwa na picha ya mtuhumiwa huyo.

Jeshi la Polisi limebaini kuwa mtuhumiwa huyo mwaka 2017 aliwahi kukamatwa kituo cha Polisi Stakishari, kupelekwa mahakamani na kupatikana na hatia ya kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha katika moja ya Mahakama ya Wilaya jijini Dar es Salaam na kuhukumiwa miaka 30 jela, baadae mwaka 2019 alikata rufaa na kutokana na sababu mbalimbali za kisheria aliweza kuachiwa.


"Mtuhumiwa huyo amefikishwa hospitali na hali yake ni mbaya" amefafanua Kamanda Muliro


Aidha Jeshi la Polisi Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za wahalifu mapema ili Jeshi la Polisi lifanye kazi ya kuzuia matukio ya kihalifu
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages