Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amelieleza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa tayari Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeanza kuandaa andiko kuhusiana na madini ya kimkakati na kuainisha aina za madini hayo kwa mtizamo wa dunia na nchi, matumizi yake na mahali yanapopatikana.
Dkt. Kiruswa amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Nusrat Hanje katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni jijini Dodoma baada ya Hanje kutaka kujua nini mkakati wa Serikali wa kuiwezesha GST kufanya tafiti za kisayansi na teknolojia kuhusu madini ya kimkakati ili kuwezesha kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa nchini.
Aidha, Dkt. Kiruswa amesema, tayari wizara imeielekeza GST kuandaa taarifa kuhusiana na uwepo wa madini hayo ikiwemo madini muhimu kwa ajili ya nishati ya kijani.
Ameeleza kuwa, GST imebaini maeneo ya kufanya tafiti za jiofisikia katika maeneo sita tofauti kwa nishati ya kijani na teknolojia pamoja na matumizi ya magari ya umeme.
Ameongeza kuwa, Serikali anaendelea kutafuta wadau wa maendeleo ambao watashirikiana katika kufanya tafiti za kisayansi.